Simanjiro. Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Mkoa wa Manyara, Samwel Gunzah ambaye ni mfungwa amefariki dunia katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, mkoani Dodoma.

Gunzah alihukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani kwa kosa la rushwa na kutumia madaraka yake vibaya Septemba 18, 2025.

Taarifa za kifo chake zilianza kusambaa mitandaoni hususan mkoani Manyara. Usiku huu wa leo Jumatatu, Machi 2, 2026, Mwananchi limemtafuta Msemaji wa Jeshi la Magereza, Elizabeth Mbezi ambaye amethibitisha kifo cha   Gunzah.

“Ni kweli alikuwa ni mgonjwa kwa kipindi kirefu na alikuwa anahudhuria Hospitali ya Mkoa wa Manyarai na akapewa rufaa kwenda Benjamin Mkapa. Umauti umemkuta katika Hospitali ya Benjamin Mkapa akipatiwa matibabu,” amesema Elizabeth.

Alipoulizwa utaratibu wa mazishi, amesema: “Taratibu zimekwisha kufanyika na ndugu wamekabidhiwa mwili kwa hatua za mazishi.”

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Makota amesema Gunzah amefariki dunia.

Amesema Gunzah ambaye alikuwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo mwaka 2021 hadi 2023 amefariki dunia mkoani Dodoma baada ya kuugua.

“Habari za kusikitisha nawafahamisha kuwa nimepokea taarifa za msiba wa ndugu yetu Gunzah aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri mwaka 2021 hadi mwaka 2023,” amesema Makota.

Gunzah alihukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani kwa kosa la rushwa na kutumia madaraka yake vibaya.

Gunzah alihukumiwa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Charles Uiso, Septemba 18, 2025, kwa kosa la kwanza la rushwa na uhujumu uchumi.

Katika hukumu hiyo Gunzah alihukumiwa miaka 20 jela kwa kosa la kwanza na miaka miwili kwa kosa la pili la kutumia madaraka vibaya, hivyo adhabu hizo ziliamuriwa kwenda sambamba.

Kwa upande mwingine, Gunzah alishinda kesi nyingine ya rushwa ya Sh5 milioni na matumizi mabaya ya madaraka, baada ya kutotiwa hatiani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *