TIMU ya Barberian, inanyemelea rekodi mbovu msimu huu katika Ligi ya Championship, baada ya kikosi hicho ambazo zamani kilikuwa kinafahamika kwa jina la Kiluvya United, kushinda mechi moja tu hadi sasa kati ya 19 ilizocheza, kikiwa mkiani.

Katika mechi hiyo moja ambayo kikosi hicho imeshinda msimu huu, ilikuwa ya ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya TMA FC kutoka jijini, Arusha, Januari 11, 2026, ila baada ya hapo imetoka sare sita na kuchapwa 12, ikibakia mkiani na pointi tisa tu.

Kwa misimu ya hivi karibuni, timu iliyoshinda mechi chache katika Ligi ya Championship, ilikuwa ni Ruvu Shooting, msimu wa 2023-2024, ambapo kikosi hicho kilishinda miwili, kikitoka sare saba na kuchapwa 21, kikimaliza mkiani na pointi 13.

Pia, Barberian ndio timu inayoongoza kwa kufunga mabao machache, ambapo hadi sasa imefunga 11, huku ikiwa nafasi ya nne kwa kuruhusu mabao mengi (31), nyuma ya B19 FC (33), Hausung FC (34) na vinara, African Sports ya Tanga iliyoruhusu 37.

Timu hiyo msimu huu ilianza kufundishwa na Moris Katumbo ‘Kamongo’, ingawa kocha huyo wa zamani wa Mashujaa Queens na Kituo cha Vijana cha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), alijiuzulu, kisha, Kheri Mohamed, kuachiwa msala huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *