WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, leo Machi 2, 2026, amekagua Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Kilutheri ya Haydom, iliyopo Wilaya ya Mbulu, Mkoa wa Manyara. Ujenzi wa jengo hilo umegharimu shilingi bilioni 6.3.

Mradi huo unalenga kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za mama na mtoto kwa kuzingatia viwango vya kisasa vya tiba, usalama wa wagonjwa, kupunguza vifo vinavyohusiana na uzazi, na kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.

Hospitali ya Kanisa la Kilutheri ya Haydom imeendelea kuwa mdau muhimu wa Serikali katika kuboresha huduma za afya ya jamii, ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma za rufaa na za kibingwa kwa wananchi wa Mkoa wa Manyara na mikoa jirani. SOMA: Waziri Mkuu ameonesha njia viongozi, watendaji waifuate

Akizungumza baada ya ukaguzi huo, Dkt. Mwigulu amesema  Rais Dk. Samia Suluhu Hassan anatambua mchango mkubwa wa madhehebu ya dini, ikiwemo Kanisa la Kilutheri, katika ustawi wa jamii.

“Serikali iliona umuhimu wa taasisi zinazofanya kazi hii zipate misamaha ya kodi kwa sababu zinachangia kuimarisha huduma za kijamii. Pia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anatambua kazi kubwa inayofanywa na watumishi katika sekta ya afya, ikiwemo hapa Haydom, kwa kuwa mnafanya kazi kubwa ya kuokoa maisha ya Watanzania,” alisema Dkt. Mwigulu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *