Dar es Salaam. Sauti yake iliposikika kwa mara ya kwanza, wengi waliiona kama ya kawaida lakini haikuchukua muda kawaida hiyo ikageuka kuwa nguvu ya kipekee.
Leo hii, jina la Zuhura Othman Soud ‘Zuchu’ limekuwa miongoni mwa majina makubwa ya wanawake waliotikisa Bongo Fleva kwa muda mfupi lakini kwa mafanikio makubwa.
Nyuma ya mafanikio hayo kuna safari ya kujithibitisha, kuvumilia maneno ya watu na kupambana ili kutoka kivulini na kusimama mwenyewe.
Kwa wasichana wengi wanaoota kuwa wasanii au kufanikiwa kwenye sekta nyingine, safari yake ni ushahidi kipaji pekee hakitoshi unahitaji moyo mgumu, nidhamu na uwezo wa kuvumilia presha.
Zuchu alizaliwa katika familia ya muziki kama ambavyo wengi wanafahamu. Mama yake ni gwiji wa taarab, Khadija Kopa, kaka yake marehemu Omar Kopa alikuwa maarufu nchini jambo lililomfanya wengi kudhani njia yake ilikuwa rahisi.
Lakini ukweli ni kuwa mtoto wa msanii mkubwa wakati mwingine ni mzigo. Watu huwatazama kwa jicho la kukulinganisha ukifanya vizuri, watasema ni kwa sababu ya jina la mzazi na ukiteleza kidogo, lawama zinakuwa mara mbili kwamba ulibebwa hukuwa na uwezo.
KATHIBITISHA UWEZO
Kabla hajawa maarufu kwenye redio na mitandao, Zuchu alithibisha uwezo wake. Alishiriki katika mashindano kama Tecno Own the Stage yaliyokuwa yanafanyika Nigeria wakati huo majaji walikuwa YemiAlade aliyekuwa anaitikisa Afrika na kibao cha Johny.
Kwenye mashindano hayo ambayo yalijaa washiriki kutoka Afrika Zuchu aliishia robo fainali lakini alifanya kazi kwa bidii na kujenga sauti yake ya kitofauti.
Wapo waliodai angeishia kuwa binti wa Khadija Kopa bila alama yake mwenyewe. Lakini hakukubali kubaki kwenye kivuli hicho na akajitengeneza mwenyewe.
“Ndiyo maana hata jina sikutaka kutumia Zuhura Kopa kwa sababu wengi wangedhani napitia kwenye kivuli cha mama yangu, kaka yangu alitumia jina hilo lakini nilitaka kujitengeneza mimi kama mimi,” anasema Zuchu.
Mwaka 2020 alipojiunga na lebo ya WCB Wasafi, chini ya msanii na mfanyabiashara Diamond Platnumz, wengi waliona kama amepewa nafasi ya bahati.
“Sikuwahi kutoa rushwa ya ngono maana kila mtu anakuchukulia kama unavyoenda, nikiwa studio nikiambiwa imba naimba wakaona nipo siriazi, msichana huwezi kukataa kutongozwa kuna wengine wanapata vishawishi ya ngono ndivyo watakavyokuchukulia.”
“Sikupewa bahati nilipambana sana mimi nimekaa Wasafi kwa miaka minne hadi mitano kuna muda nilikuwa namwambia kaka yangu nataka niache muziki niendelee na mengine.”
Anaongeza “Nimepambana sana hadi watu wananiona nimevumilia vya kutosha kuna kipindi nilipeleka nyimbo tano kwa Diamond zote alizikataa.”
Hata hivyo, kilichofuata ndicho kilichowanyamazisha baadhi ya wakosoaji. Ndani ya muda mfupi, aliachia nyimbo zilizotikisa kama ‘Wana’, ‘Sukari’, ‘Nisamehe’ na ‘Nobody’ na kuanza kuvunja rekodi za watazamaji kwenye mtandao wa YouTube.
Kwa mara ya kwanza ndani ya kipindi kirefu, Bongo Fleva ilipata msanii wa kike aliyekuwa anaongoza kwa namba, si kwa kubahatisha wala kubebwa bali kwa ushindani halisi wa soko.
Ndani ya muda huo Zuchu aliandika rekodi ya kuwa msanii wa kwanza wa kike Tanzania na Afrika Mashariki video ya wimbo wa Sukari kufikisha watazamaji zaidi ya Milioni 100.
Rekodi nyingine EP yake ya I Am Zuchu (2020) ilifanya vizuri hadi kumwezesha kushinda tuzo ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) kama Msanii Bora Chupukizi.
PRESHA YA UMAARUFU
Lakini mafanikio huja na changamoto zake, Kadri jina lake lilivyokua, ndivyo mijadala ya mitandaoni ilivyozidi kuwa gumzo. Maisha yake binafsi, mahusiano, mavazi, hata maneno yake yalifuatiliwa kwa ukaribu.
Kuna wakati alikumbansa na maneno makali na kejeli, lakini alisimama kidete. Aliendelea kutoa muziki, kufanya maonyesho na kushirikiana na wasanii wa ndani na nje ya nchi. Hapo ndipo funzo kubwa linapojitokeza kwa wasichana wengi huwezi kuwazuia watu kuzungumza, lakini unaweza kuamua mazungumzo hayo yasikuzuie kusonga mbele.
“Kusema ukweli haikuwa inanipa shida maneno ya watu kwa sababu Wasafi inajulikana kwa kiki na hiyo ni biashara, watu wanapitia stresi wanauguza watu wao kuna muda inabidi wakipita kwenye peji za udaku wakutane na kitu kutoka kwako kwa hivyo ni vitu vya kawaida nadhani.”
Tasnia ya muziki Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikitawaliwa na wanaume wengi. Wasanii wa kike mara nyingi hukumbana na changamoto za kuonekana kama wanapitia kwenye migongo yao, badala ya wabunifu. Zuchu aliingia kwenye soko hilo hilo, akashindana kwa kazi na ubunifu.
“Mimi nilikuwa nashindanishwa na wanaume kwenye lebo wakina Lavalava na kushindanishwa kulikuwa kunanisumbua lakini kulinifunza kwa sababu wanaume wanaandika vizuri zaidi kuliko sisi wanawake.”
Kutokana albamu na nyimbo zake, ameonyesha uwezo wa kuimba, kuandika na kuwasilisha hisia zinazogusa rika tofauti. Nyimbo zake za mapenzi zimewafanya wengi kujiona ndani ya simulizi zake. Hilo limekuwa silaha yake, uwezo wa kuunganisha sauti na hisia za jamii.
“Nilitamani kila ninachoandika kiwafikie rika lote sio siku zote niwaimbie watoto kuna nyimbo za watu waliopo kwenye penzi zito lazima niwaburudishe.”
Zaidi ya hapo, amekuwa miongoni mwa wasanii wa kike waliotazamwa zaidi Afrika Mashariki, jambo linalothibitisha kuwa mwanamke anaweza kuongoza soko bila kupewa nafasi ya upendeleo.
Mwanadada huyo ndiye mwanamuziki wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kazi zake kutazamwa YouTube zaidi ya mara bilioni moja, akiweka rekodi hiyo miaka sita tangu amesainiwa Wasafi.
KAVUNJA DHANA POTOFU
Kuna dhana kwamba mafanikio ya haraka hayadumu. Lakini kwa zaidi ya miaka kadhaa sasa, Zuchu ameendelea kubaki juu ya ramani ya muziki. Amefanikiwa kujenga brand yake binafsi kutoka muziki, mitindo hadi ushawishi wa kibiashara.
Kwa wasichana wanaotoka kwenye familia zenye majina makubwa, simulizi yake inatoa ujumbe muhimu kuwa jina linaweza kufungua mlango, lakini ni wewe utakayeamua ubaki ndani ya chumba hicho au utoke nje. Zuchu aliamua kubaki na kupambana.
SOMO KWA KIZAZI KIPYA
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo kilele chake hufanyika Machi 08 kila mwaka, simulizi ya Zuchu inagusa eneo muhimu uhuru wa mwanamke kuchagua ndoto yake na kuipigania. Si lazima uwe mkamilifu mbele ya jamii, Si lazima watu wote wakuelewe muhimu ni kujua unachotaka na kukifanyia kazi.
Wasichana wengi hukata tamaa wanapokutana na maneno ya kukatisha tamaa kutoka kwa watu wa karibu au mitandaoni. Lakini mfano wa Zuchu unaonyesha kuwa kukosolewa sio mwisho wa safari wakati mwingine ni ishara kwamba unafanya jambo linaloonekana.
Safari yake pia ni darasa la kujifunza kuhusu nidhamu ya kazi, kuachia wimbo mmoja mzuri ni rahisi lakini kudumisha kiwango ni kazi, Zuchu ameonyesha uthubutu wa kutoa kazi nzuri mfululizo, kushiriki maonyesho na kuendelea kujiboresha. Katika mazingira ambayo ushindani ni mkubwa na ladha za mashabiki hubadilika haraka, kubaki juu kunahitaji zaidi ya kipaji. Inahitaji kujitambua na kujisimamia.
Jina la Zuchu linabeba ujumbe mzito kwa kizazi kipya kwamba sio lazima utoke kwenye mazingira magumu sana ili uonekane shujaa, wakati mwingine changamoto ni matarajio makubwa ya watu juu yako.
Kutoka kuwa binti wa Khadija Kopa hadi kuwa nyota anayejitegemea, Zuchu ameandika ukurasa wake mwenyewe katika historia ya Bongo Fleva. Na kwa wasichana wanaosoma simulizi yake, funzo ni moja tu ndoto yako ni halali, sauti yako ni muhimu, na nafasi yako ipo. Usikate tamaa amini siku yako inakuja.