Dodoma. Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), wametaja sababu za wagonjwa wengi hasa madereva wa bodaboda au abiria wao kukatwa sehemu ya viungo vyao, ni kuchelewa kufika kwenye huduma.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Machi 2, 2026 na Mkurugenzi wa MOI, Dk Mpoki Ulisubisya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utendaji kazi wa taasisi hiyo.
Kumekuwa na taarifa zisizothibitishwa kuwa, madereva bodaboda wakifikishwa MOI kama wamepata ajali na kuvunjika miguu au mikono, tiba yao huwa ni kukatwa viungo.
Katikati ya uvumi huo, taasisi hiyo hivi karibuni iliibuka mshindi miongoni mwa hospitali zilizotoa huduma bora kwa wagonjwa wa mivunjo ikifuatiwa na Hospitali ya rufaa ya Dodoma, kwenye tuzo zilizotolewa na mtandao wa watengenezaji vyuma vya kutibia mifupa ya nchini Marekani.
Dk Ulisubisya amesema kauli hizo ni mitazamo ya watu lakini hazina ukweli kwani wao wanafanya kazi kwa maadili na viapo vya kitaaluma.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Balozi Dk Mpoki Ulisubisya akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dodoma
“Shida ni moja, mtu anapata ajali halafu anachelewa kuja hospitali na akija sehemu ya kiungo hicho imeanza kuharibika, kipi bora umuache apoteza maisha ama utoe kiungo hicho awe salama,” amesema Dk Ulisubisya na kuongeza;
“..sasa kwa sababu kule mtu alifungiwa hapa tukimkata ndiyo taarifa kuwa pale MOI wanagombania kama mpira wa kona kwa ajili ya kukata tu, siyo kweli,” amesema.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo amesema baadhi ya matibabu ni gharama na iwapo Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote utabeba magonjwa yote, ni wazi kuwa utafilisika hata kabla ya kufikisha miaka miwili.
Amesema yako baadhi ya magonjwa ikiwemo upasuaji wa ubongo vifaa vyake ni gharama kubwa akashauri hadi kama nchi wanachama watakubali kuagiza kwa wakati mmoja huenda itasaidia.
Akizungumzia huduma katika taasisi hiyo, amesema ndani ya kipindi cha miezi 12 walihudumia wagonjwa 180,000 ambapo miongoni mwao 500 walitoka nje ya nchi.
Kwenye idadi hiyo wagonjwa 2,300 walipata huduma bobezi ikiwemo waliotibiwa kupitia teknolojia ya akili unde (AI) ambayo sehemu kubwa ilitumika kwenye matibabu ya upasuaji ubongo na mgongo.
Amefafanua kuwa taasisi hiyo inapokea wagonjwa kati ya 500 hadi 800 na kwa sasa wanaongeza majengo mengine ikiwemo jengo la kuhudumia watoto mahututi ili wasiwachanganye na watu wazima.
Taasisi hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1996, imeongeza huduma tisa katika kipindi kifupi ikiwemo za kuunga vipande vya mgongo vilivyosagika, viungo vilivyopooza na kamba za kuunganisha misuli na mifupa.