MUFTI na Shehe Mkuu wa Tanzania, Dk Abubakar Zubeir, amesema mashindano ya kimataifa ya Quran Tukufu yanayoandaliwa na Taasisi ya Al-Hikma yameipa Tanzania heshima kubwa kimataifa.

Mufti Zubeir ameyasema hayo  jijini Dar es Salaam wakati wa mashindano ya Quran  ambapo amesema zamani haikuwa rahisi kwa watu wa nje kuitaja Tanzania kutokana na tukio la aina hiyo, lakini sasa mashindano hayo yameifanya Tanzania kutambulika duniani.

“Zamani ilikuwa vigumu mtu kwenda nje na kutajiwa Tanzania kwa sifa kama hii, lakini sasa ukienda popote utaona watu wakitaja tukio hili na kufurahishwa na mkusanyiko pamoja na usimamizi wake,” alisema.

Ameipongeza Taasisi ya Al-Hikma kwa maandalizi mazuri ya mashindano hayo na kueleza kuwa hata yeye binafsi amekuwa akipokea pongezi kutokana na tukio hilo. “Nimpongeze Shehe Sharif Abdulqadir Al-Ahdal na Nurdeen Kishki kwa maandalizi haya makubwa yaliyofanikisha tukio hili lenye heshima kubwa kwa Watanzania na Waislamu kwa ujumla,” alisema.

Pia aliwasihi Waislamu kuitumia fursa hiyo kuzingatia mafundisho ya Qurani na kuyatekeleza katika maisha yao ya kila siku. Kwa upande wake, SOMA: Rais Samia atoa Sh Mil 10 washindi mashindano ya Quran

Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa amesema taasisi hiyo imeendelea kuliheshimisha taifa kwa kuandaa mashindano ya kimataifa yanayovutia washiriki na watazamaji kutoka sehemu mbalimbali duniani. “Hii ni heshima kwa Watanzania na kwa taasisi yenyewe pamoja na Waislamu wanaoitikia wito wa kushiriki mashindano haya. Leo tumepata washiriki 16 kutoka mabara mbalimbali duniani,” alisema.

Katika mashindano hayo, Mwenyekiti wa mashindano hayo, Shehe Kishki, amewatangaza washindi ambapo mshiriki kutoka Uganda, Abdulrahman Yassin, aliibuka mshindi wa kwanza na kujishindia Sh milioni 30. Nafasi ya pili ilichukuliwa na Mohamed Mustafa kutoka Canada aliyepata Sh milioni 20, huku mshindi wa tatu akiwa Shoaib Mohamed kutoka Sweden aliyepata Sh milioni 12.5.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *