Mbuni ang’ara shindano la ndege wa mwakaMbuni ang’ara shindano la ndege wa mwaka

SHIRIKA lisilo la kiserikali (NGO) la Nature Tanzania linalojihusisha na uhifadhi wa viumbe hai nchini limemtangaza mbuni kuwa Ndege wa Mwaka 2026 Tanzania baada ya kupata kura 303 zilizopigwa mwaka jana. Ndege wengine waliokuwa wakishindana katika kampeni hiyo ni Tandawala Mkubwa, Kwale Shingo Nyekundu na Southern Hornbill.

Akizungumza wakati wa kutangaza mshindi katika Shule ya Msingi Manyara Ranch iliyopo Makuyuni wilayani Monduli mkoani Arusha mwishoni mwa wiki, Ofisa Uanachama na Masoko wa Nature Tanzania, Gaudentia Mariki, alisema mbuni alipata kura 303, ambapo kura 186 zilipigwa kwa njia ya mtandao na kura 117 zilipigwa na wananchi ana kwa ana.

Mariki amesema ndege wote wanne waliokuwa kwenye shindano hilo wanapatikana katika ardhi za malisho na walipewa kipaumbele kutokana na kaulimbiu ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa (UN) inayotambua mwaka 2026 kuwa mwaka maalumu kwa wafugaji na ardhi za malisho.

“Sifa zilizomfanya mbuni aibuke mshindi wa mwaka 2026 ni pamoja na kuwa ndiye ndege mkubwa kuliko wote duniani, anakimbia ardhini, anaishi na kutaga mayai ardhini na hana uwezo wa kuruka kama ndege wengine, jambo linalomfanya kuwa wa kipekee,” alisema Mariki.

Ameongeza kuwa kupitia sifa hizo, mbuni anaweza kutumika kama mwakilishi wa uhifadhi wa maeneo ya ardhi za malisho kwa kuwa hupatikana zaidi katika maeneo hayo ya wazi na tambarare yenye vichaka vichache na majani mengi. SOMA: Ruhila; Bustani ya wanyamapori iliyojaa fursa za uwekezaji, utalii

Mariki amesema kupitia kampeni ya Ndege wa Mwaka, wataweza kukusanya taarifa mbalimbali kuhusu mbuni, ikiwemo maeneo wanakopatikana na idadi yao, jambo litakalosaidia katika juhudi za uhifadhi. “Kipindi cha kupiga kura tulikusanya maoni kupitia mada iliyosema ‘Ardhi za malisho si jalala’. Tunatarajia kampeni ya mwaka 2026 itawafikia wafugaji wengi na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kulinda ardhi,” alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Utalii wa Wilaya ya Monduli, Jonas Nyange, amesema katika taswira ya utalii mbuni ni ndege anayevutia kwa sababu jike ana rangi ya kijivu na dume ana rangi nyeusi. “Kwa mfano, jike anapotaga mayai, mchana huatamia, na usiku huatamia dume kwa kuwa ana rangi nyeusi, hivyo haonekani kwa urahisi kwa adui,” alisema Nyange.

Ameongeza kuwa mbuni ana shingo ndefu na vidole viwili vinavyomsaidia kukimbia kwa kasi, hali inayowavutia watalii wanapomuona katika maeneo ya nyika. Wenyeviti wa Kijiji cha Esilalei, Laigwanani Leeko Tayal na Laigwanani Tobiko Lesiara, walisema mbuni ni ndege muhimu kwa jamii ya Wamasai.

Walisema wakati wa kuwapeleka vijana jandoni, huvalishwa manyoya ya mbuni aliyedondosha manyoya yake kama ishara ya nguvu na uzazi. Aidha, walisema wataalamu wa Kimasai hutumia manyoya ya mbuni katika ibada za kuomba mvua wakati mvua zinapochelewa kunyesha, na ni mwiko kutumia manyoya ya mbuni aliyekufa katika jando au mila nyingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *