Morogoro. Zaidi ya kaya 700 zimekumbwa na mafuriko baada ya mto Mbulumi kuvunja kingo zake na kuelekeza maji katika makazi ya watu, hali iliyosababisha nyumba zaidi ya 20 kubomoka na wananchi kulazimika kukimbia makazi yao kuokoa maisha.
Wananchi walioathirika na mafuriko hayo sasa wanaomba msaada wa haraka wa chakula, mavazi na makazi, pamoja na hatua za kudhibiti mto Mbulumi uliopoteza mkondo wake wa asili.
Wakizungumza na Mwananchi leo Machi 2.2026 wilayani Mvomero mkoani Morogoro, wananchi wameeleza kuwa mafuriko hayo yameharibu mali mbalimbali za wakazi wa kijiji cha Kichangani alfajiri ya Februari 23, 2026 baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha mto Mbulumi kufurika maji kisha kuvunja kingo na kuingia katika makazi ya wananchi.
Mkazi wa kitongoji cha Msufini, kijiji cha Kichangani, kata ya Mhonda, wilaya ya Mvomero, Mariam Mhando (55), akiwa amekaa katika kizingiti cha nyumba yake iliyojaa maji baada ya mafuriko kuingia katika makazi ya wananchi na kuharibu mali mbalimbali mkoani Morogoro. Picha na Juma Mtanda.
Mtoto wa, Salum Samagubi, Mwantumu Haji (35), amesema licha maji ya mafuriko kuharibu mali mbalimbali familia yao imeachwa na kumbukumbu mbaya ya nyumba kubomoka.
Baada ya maji mengi kuvamia nyumba zao, baba yao akiwa ndani ya nyumba akiugulia maumivu ya homa aliokolewa muda mfupi kabla ya nyumba kudondoka.
Mwantumu amesema mzazi wake hakuwa anajua lolote kuhusu nini kinaendelea nje.
“Ilipofika saa moja asubuhi maji yaliingia kwa kasi ndani ya nyumba na kuzingira makazi yetu na majirani, wakati huo baba yangu ni mgonjwa na hakuwa anaelewa kinachoendelea. Mume wangu aliingia haraka ndani ya nyumba kumtoa. Dakika chache baada ya kutoka nje, nyumba yote ilianguka,” amesema Mwantumu.
Ameongeza kuwa kama kungekuwa na kuchelewa hata kwa dakika mbili, huenda baba yake angefunikwa na kifusi na kupoteza maisha. “Tulipoteza mahindi, nguo na vifaa vyote vya ndani,” amesema.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Msufini, Saidi Kizumi (63), amesema mafuriko hayo yalianza saa 10 alfajiri baada ya mto Mbulumi kupoteza mkondo wake wa asili na kuelekeza maji katika makazi ya watu.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Msufini, kijiji cha Kichangani, kata ya Mhonda, wilaya ya Mvomero, Saidi Kizumi, (kushoto) akikagua moja ya nyumba za ibada zilizozingirwa na maji baada ya Mto Mbulumi kupoteza mkondo wake wa asili na kusababisha mafuriko kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani Morogoro. Picha na Juma Mtanda.
“Kaya 720 zilizingirwa na maji na nyumba zaidi ya 20 zilibomoka kabisa. Taarifa zilitolewa kwa viongozi wa kijiji, kata na wilaya, ndipo askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji walipofika kusaidia uokoaji, hasa kwa wazee na wagonjwa,” amesema Kizumi.
Ameongeza kuwa mkuu wa wilaya ya Mvomero alifika kukagua hali ya waathirika na kuagiza wananchi walioathirika wahamishiwe katika eneo la Shule ya Msingi Kichangani kama makazi ya muda wakati taratibu nyingine zikiendelea.
Kwa mujibu wa Kizumi, madhara ya mafuriko hayo ni makubwa, yakihusisha uharibifu wa vyakula, mifugo, mazao mashambani na mali nyingine, hali iliyoyumbisha uchumi wa kaya nyingi.
“Mto umeacha njia yake ya asili na sasa unaelekeza maji moja kwa moja kwenye makazi ya watu. Tunahitaji msaada wa haraka na suluhu ya kudumu,” amesema.
Mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Kichangani, Lisa Juma (11), akiwa na mwenzake wakianika vitabu vilivyoathiriwa na mafuriko baada ya maji kuingia katika nyumba zao, kitongoji cha Msufini, kijiji cha Kichangani, kufuatia Mto Mbulumi kupoteza mkondo wake wa asili mkoani Morogoro. Picha na Juma Mtanda.
Mkazi wa Msufini, Amini Juma, amesema chanzo kikuu cha mafuriko ni kuondolewa kwa daraja dogo lililokuwa likitumiwa na wananchi baada ya kujengwa daraja kubwa katika mto Mbulumi, akisema daraja hilo dogo lilikuwa likipunguza kasi ya maji kabla ya kuvunjwa kwa hofu ya usalama.
Pia ametaja kuzibwa kwa lango la maji lililokuwa likiyaelekeza kwenye mashamba ya miwa ya kiwanda cha Mtibwa Sugar, hali iliyosababisha kubadili mkondo na kuingia katika makazi ya wananchi.
“Serikali ikileta skaveta kufukua mto na kufungua njia ya maji, tatizo litapungua. Lakini pia lango la maji linaloelekea mashamba ya miwa lifunguliwe,” amesema.
Mkazi mwingine, Judith Frank (46), amesema mafuriko yamekuwa yakiwasumbua kwa zaidi ya siku tano, akidai kulikuwa na mwekezaji aliyekuwa tayari kuchimba mchanga ili kuongeza kina cha mto, lakini alizuiwa na viongozi wa kijiji na kata.
“Kama angeachwa, maji yangepita kwa uhuru,” amesema.