Kama kuna muujiza wa soka unaondelea duniani kwa sasa basi ni klabu ya FK Bodø/Glimt ya Norway.
Ikishiriki ligi ya mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza, klabu hiyo hiyo imefanya kile ambacho mtu asingeweza kuamini kingetokea wakati msimu unaanza.
Ushindi wa jumla wa mabao 6–2 dhidi ya Sturm Graz ya Austria kwenye hatua ya kufuzu, ulionekana wa kubahatisha wakati ule.
Lakini walichokifanya kwenye hatua ya makundi ndicho kilichowaacha wengi mdomo wazi.
Kiungo wa Bodo/Glimt, Håkon Evjen, akishangilia moja ya bao katika ushindi wa 2-1 iliopata timu yake dhidi ya Inter Milan katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Mtandao
Walianza kwa kuwachapa Manchester City 3-1, wakaja kuichapa Atlético Madrid 2-1 na sasa wamerudia tena jeuri yao kwa wakubwa kwa kuitupa nje Inter Milan na kufuzu hatua ya 16 Bora.
Ukirejea walichokifanya dhidi ya Atletico Madrid dimbani Wanda Metropolitano, basi unaweza kuwaonea huruma Inter Milan. FK Bodø/Glimt ni kielelezo cha kukua kwa soka la Norway hivi sasa. Ukiyaangalia kwa umakini mambo yanavyoindea vizuri Norway kwa sasa, unaweza kusema huu ni wakati wao.
Hadi sasa, Norway, inaongoza kwa kuzoa medali nyingi katika Olimpiki ya majira ya baridi inayoendelea huko Italia. Picha na Mtandao
WANAONGOZA KWENYE OLIMPIKI
Hivi sasa huko Italia kwenye miji ya Milan na Cortina d’Ampezzo, michezo ya XXV ya Olimpiki ya majira ya baridi inaendelea. Olimpiki ya majira ya baridi ni maalumu kwa nchi zenye baridi kali duniani.
Norway hadi sasa inaongoza kwa kuzoa medali nyingi. Hadi wakati makala hii inaandikwa, Norway walikuwa tayari wamezoa medali 37 za ujumla.
Kati ya hizo; 17 za dhahabu, 10 za fedha na 10 za shaba.Anayefuata ni Marekani mwenye jumla ya medali 27, kumi nyuma ya Norway. Kati ya hizo; 9 za dhahabu, 12 fedha na 6 za shaba.
Michezo ya mwaka huu imekuwa gumzo kubwa sana baada ya kuzagaa kwa taarifa za matumizi ya kihistoria ya mipira ya kiume.
Kwa kawaida waandaaji wa michezo huyo hugawa mipira ya kiume kwa wanamichezo ili wajiepushe na ngono zembe.
Mwaka huu umetia fora, hadi siku tatu za kwanza tayari mipira 10,000 ilishagawiwa na kuwafanya wagawaji kuishiwa akiba.
Kwenye mashindano kama haya ambayo hukutanisha wanamichezo vijana wanaochemkwa na damu, mahusiano hayaepukini.
Wanamichezo hawa kutoka mataifa mbalimbali duniani hujikuta wakikaa kambi ndani ya kijiji kimoja cha michezo, baada ya kutoka kwenye maandalizi ya muda mrefu na yenye kuwatenga na maisha ya kawaida.
Pale sasa ni kama wametoka vifungoni, ndiyo maana waandaaji hugawa mipira hiyo wakijua lazima kutakuwa na ‘vurugu’. Na kwa kasi ya matumizi ya mipira mwaka huu, yawezekana ni hawa hawa Norway ndio vinara!!!
Mshambuliaji wa Norway, Erling Haaland ambaye pia anakipiga Man City ya England. Picha na Mtandao
MTU HATARI KWA NYAVU
Norway ndio nchi anakotoka mfumania nyavu hatari zaidi duniani kwa sasa, Erling Haaland. Kwenye Ligi Kuu ya England hadi sasa ana mabao 22 kwenye mechi 26 alizocheza. Kwenye ligi ya mabingwa Ulaya, ana mabao 7 kwenye mechi 8 hadi sasa. Yaani kwa ujumla ana mabao 29 kwenye mechi 36, hebu dhania!
Baadhi ya wachezaji wa Norway, wakishangilia baada ya kufuvu kushiriki Kombe la Dunia la 2026. Picha na Mtandao
WAMEFUZU KOMBE LA DUNIA 2026
Ushindi wa kishindo wa mabao 4-1 dhidi ya Italia uliomfanya kocha wa Italia, Gennaro ‘Rhino’ Gattuso kulalamika kama mtoto, uliwapa Norway tiketi ya kwanza ya Kombe la Dunia baada ya miaka 28.
Mara ya mwisho Norway kufuzu Kombe la Dunia ilikuwa 1998 nchini Ufaransa ambapo moja ya kumbukumbu zao ni kuivunja moyo Afrika.
Walishinda 2-1 dhidi ya Brazil na kukatisha matumaini ya Morocco kufuzu 16 bora licha ya ushindi wa kishindi wa 3-0 dhidi ya Scotland.
Bao la ‘jioni’ la Norway likaitupa nje ya mashindano Morocco ambazo zilikuwa kundi moja. Tangu hapo hawakufanikiwa tena kufuzu hadi sasa wanapofuzu tena.
Filamu kutoka Norway ya Sentimental Value, ambayo ilishinda tuzo ya Oscar katika kipengele cha picha bora. Picha na Mtandao
FILAMU BORA
Kwenye tuzo za Oscars kwa ajili ya filamu bora, filamu kutoka Norway, Sentimental Value, imetajwa kuwania kipengele cha picha bora.
Kwa namna ilivyo, filamu hiyo ina nafasi kubwa sana ya kushinda kipengele chake.
Na kama itakuwa hivyo, basi utakuwa muendelezo wa mambo kuinyookea nchi hiyo ya Scandinavia.
Ama kwa hakika mwaka ukiwa wako, kila unachogusa hugeuka dhahabu ndivyo ilivyo kwa Norway. Huu ni wakati wao!