Marekani. Licha ya kwamba mwenyewe alishafariki dunia tangu Juni 25, 2009, lakini Michael Jackson ‘Wacko Jacko’ amefunguliwa mashtaka.

Ndiyo, watu wanne ndugu wa familia moja wamefungua kesi ya kudai mali dhidi ya marehemu Mfalme wa Pop, Michael Jackson kutokana na kuwanyanyasa kingono walipokuwa watoto.

Kwa mujibu wa hati ya madai iliyowasilishwa Februari 27 na kunukuliwa na jarida la People, ndugu hao  Edward, Dominic, Marie Nicole na Aldo Cascio walidai Jackson alitumia umaarufu wake, utajiri pamoja na mtandao wa wafanyakazi na washauri wake kukaa karibu nao na kupata imani ya familia yao.

Katika hati hiyo ya kurasa 23, wamesema walikutana na Jackson kutokana na baba yao aliyekuwa meneja katika hoteli ya kifahari jijini New York ambako msanii huyo alikuwa akifikia mara kwa mara miaka ya 1980.

Baada ya kujenga urafiki na familia hiyo kwa zawadi, ukarimu na ukaribu wa mara kwa mara, wanadai aliwatenga na watu wazima wengine, akawapa pombe na dawa za kulevya, kuwaonyesha picha chafu na kuwanyanyasa kila mmoja wao kivyake.

“Michael Jackson alikuwa mnyanyasaji wa watoto wa muda mrefu ambaye kwa zaidi ya muongo mmoja aliwadanganya, kuwapa dawa, kuwabaka na kuwashambulia kingono wadai wote, baadhi yao wakiwa na umri wa miaka saba au nane,” sehemu ya hati hiyo ilieleza.

Ndugu hao wamesema unyanyasaji huo ulitokea katika maeneo mbalimbali duniani, ikiwemo nyumbani kwa familia hiyo, katika safari za kimataifa pamoja na makazi ya Jackson ya Neverland Ranch yaliyoko California.

Hata hivyo, upande wa mtetezi wa Jackson, Wakili Marty Singer amepinga vikali madai hayo na kesi hiyo ni jaribio la kutafuta fedha kwa njia ya mkato.

“Kesi hii ni njama ya kutafuta mamia ya mamilioni ya dola kutoka kwenye mali na kampuni za Michael,” amesema Singer

Aliongeza, familia hiyo kwa zaidi ya miaka 25 ilimtetea Jackson hadharani na kuthibitisha hakuwa na tabia za kuwachezea watoto sasa kwa nini wabadilike.

Singer pia alidai kauli za familia hiyo katika kitabu cha Frank Cascio cha mwaka 2011 na mahojiano mbalimbali, ikiwemo yale aliyofanya na Oprah Winfrey, zinakinzana na madai mapya aliyowasilishwa mahakamani.

Kwa upande wao, ndugu hao wamesema walikaa kimya kwa muda mrefu kutokana na hofu, aibu na kile walichodai ni mikataba ya kifedha iliyolenga kuwanyamazisha.

Hivi karibuni walifika katika mahakama ya Beverly Hills kwa ajili ya usikilizwaji wa makubaliano ya kifedha waliyoyataja yasiyo halali na yaliyolenga kuwanyamazisha wahanga wa unyanyasaji wa utotoni.

Katika mahojiano na gazeti la Daily Mail, mmoja wa ndugu hao Aldo Cascio mwenye umri wa miaka 35, alidai unyanyasaji wake ulianza akiwa na miaka saba.

Amesema alihisi kuchanganyikiwa na kuamini kuwa kile kilichokuwa kinafanyika ni upendo, baada ya kuaminishwa hivyo na Jackson.

Jackson alifariki dunia mwaka 2009 akiwa na umri wa miaka 50. Tangu kifo chake, kumekuwa na madai na kesi kadhaa zinazohusu tuhuma za unyanyasaji wa kingono, huku watu wa marehemu wakiendelea kuyakanusha vikali.

Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea kusikilizwa wiki zijazo kuona hatma ya madai hayo mazito dhidi ya jina la mmoja wa wasanii wakubwa kuwahi kutokea katika historia ya muziki wa dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *