Riyadh, Saudi Arabia. Nahodha wa Ureno, Cristiano Ronaldo, anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya haraka kubaini ukubwa wa majeraha ya misuli aliyoyapata katika mchezo wa klabu yake ya Al-Nassr dhidi ya Al-Fayha mwishoni mwa wiki ambapo timu yake ilichomoza ushindi wa mabao 3-1.

Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, alilazimika kutolewa uwanjani dakika 10 kabla ya mechi kumalizika baada ya kuashiria benchi kuwa alikuwa amehisi maumivu. Alionekana akichechemea wakati akitoka uwanjani na baadaye akaonekana akiwa amewekewa barafu mguuni.

Tukio hilo limeibua hofu kwa mashabiki wa Ureno huku Kombe la Dunia likiwa limebakiza miezi mitatu kuanza. Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa ya sita na ya mwisho kwa Ronaldo katika historia yake ya soka.

Kocha wa Al-Nassr, Jorge Jesus, amesema Ronaldo alipata maumivu ya misuli na  madaktari wa timu watafanya vipimo vya haraka kujua zaidi hali yake. Picha na Mtandao

Kocha wa Al-Nassr, Jorge Jesus, amesema mshambuliaji huyo alipata maumivi ya misuli na kwamba madaktari wa timu watafanya vipimo vya dharura kubaini hali yake.

Katika mechi hiyo, Ronaldo alipata nafasi ya kuipa Al-Nassr bao la kuongoza mapema dakika ya 12 kufuatia mchezaji mwenzake, Mohamed Simakan kuchezewa rafu ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo, penalti yake ilipita nje ya lango.

Hiyo ilikuwa penalti ya 35 kuikosa tangua aanze kucheza soka, akiwa tayari amefunga penalti 181 kati ya 216 alizopiga.

Nahodha huyo wa Al-Nassr na Ureno, hadi sasa amebakiza idadi ya mabao 35 kufikia rekodi ya mabao 1,000.

Mshambuliaji wa Al-Nassr, Cristiano Ronaldo, wakati akipiga mkwaju wa penalti ambao ulipita nje ya lango katika mechi ya Ligi Kuu Saudi Arabia dhidi ya Al-Fayha. Picha na Mtandao

Mechi zapigwa kalenda mpya

Wakati huo huo, mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Asia kati ya Al-Nassr na klabu ya Al-Wasl ya Falme za Kiarabu imeahirishwa kutokana na mvutano unaoendelea Mashariki ya Kati.

Shirikisho la Soka la Asia (AFC) limesema limechukua uamuzi huo kwa kuzingatia hali ya usalama kufuatia mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani na Israel dhidi ya Iran, na hatua za kulipiza kisasi zilizoripotiwa kufanywa na Iran.

Katika taarifa yake, AFC imesema mechi za ukanda wa Magharibi katika mashindano yake mbalimbali zitaahirishwa hadi itakapotangazwa, huku mechi za ukanda wa Mashariki zikiendelea kama ilivyopangwa.

AFC imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya usalama ili kuhakikisha wachezaji, maofisa na mashabiki wanakuwa salama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *