Serikali, Lifezone wajadili Mradi wa KabangaSerikali, Lifezone wajadili Mradi wa Kabanga

MSAJILI wa Hazina,Nehemiah Mchechu, amekutana na Mwanzilishi na Mwenyekiti wa kampuni ya Lifezone Metals Limited, Keith Liddell, kujadili maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Kabanga Nickel unaotekelezwa kwa ubia na Serikali ya Tanzania.

Mazungumzo hayo yalifanyika Jumatatu, Machi 2, 2026, katika Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam, yakilenga kujadili hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo uliopo mkoani Kagera wenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 2.5.

Akizungumza katika mkutano huo, Mchechu amesema Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unatekelezwa kwa kuzingatia uwazi, uwajibikaji na tija kwa manufaa ya wananchi.Amesema ushirikiano kati ya Serikali na wawekezaji unaonesha dhamira ya dhati ya kuendeleza rasilimali za nchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, Liddell ameeleza kuridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa katika hatua ya awali kabla ya kufanyika kwa Uamuzi wa Mwisho wa Uwekezaji (Final Investment Decision – FID) unaotarajiwa kufanyika mwaka huu, 2026. Amesisitiza kuwa kampuni yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania kuhakikisha mradi huo wa kimataifa unatekelezwa kwa mafanikio.

Mradi wa Kabanga Nickel ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta ya madini nchini na unatarajiwa kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha uzalishaji wa nickel duniani.Kwa mujibu wa upembuzi yakinifu uliokamilika Julai 2025, mgodi wa Kabanga ni miongoni mwa machimbo makubwa yenye kiwango cha juu cha madini ya nickel sulfidi duniani yaliyo tayari kuendelezwa.

Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuongeza ajira kwa Watanzania, kukuza ujuzi wa ndani, kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa. Aidha, mradi huo utaimarisha mnyororo wa thamani katika sekta ya madini na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa. SOMA: Mavunde aagiza mradi wa Kabanga Nickel kutekelezwa kwa wakati

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *