KAMPUNI ya Mbolea Tanzania (TFC) imesema tani 20,000 za mbolea ya kukuzia aina ya Urea zinatarajiwa kuingia nchini wiki hii kutoka Uturuki kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima katika msimu huu wa kilimo.

Mkurugenzi Mkuu wa TFC, Samuel Mshote, aliiambia HabariLEO kuwa hadi sasa kampuni hiyo imeingiza na kusambaza tani 26,000 za mbolea ya kukuzia aina ya Urea. “Tunatarajia tani 20,000 ziingie nchini wiki hii na tutazisambaza kwa wakulima. Hatuna uhaba wa mbolea na tunaendelea kuwafikia wakulima katika maeneo yote nchini,” alisema Mshote.

Amesema kwa sasa TFC inaendelea kusambaza tani 10,000 za mbolea ya kunenepesha mazao aina ya CAN kwa wakulima katika maeneo mbalimbali nchini. Mshote amesema tangu kuanza kwa msimu wa kilimo mwishoni mwa mwaka jana, TFC imeingiza na kusambaza tani 50,000 za mbolea ya kupandia aina ya DAP kwa wakulima wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na mikoa ya Tabora na Kanda ya Ziwa.

“Malengo yetu yalikuwa kusambaza zaidi ya asilimia 60 ya mbolea hiyo na tumefanikiwa. Kwa sasa tunaendelea kuwahudumia wakulima wa kanda nyingine ambako msimu wa kilimo unaendelea au umeanza,” alisema.

Ameongeza kuwa katika Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, usambazaji wa mbolea ya kupandia unaendelea. Mshote amesema TFC ina vituo 18,000 vya mauzo na mwaka huu imeboresha mfumo wa usambazaji kwa kufungua maghala kwa kushirikiana na vyama vya ushirika na vikundi vya wakulima.

Aidha, amesema kampuni hiyo ina magari ya tani 10 yanayobeba mifuko 200 ya mbolea, kila mfuko ukiwa na kilogramu 50, ambayo yamegeuzwa kuwa vituo vya mauzo vinavyotembea ili kurahisisha huduma kwa wakulima. Amesema TFC inatumia mawakala zaidi ya 600 waliosajiliwa pamoja na vyama vya ushirika 29 kusambaza mbolea kwa wakulima nchini.

Mshote amesema hatua hizo zinasaidia wakulima kupata mbolea kwa bei elekezi yenye ruzuku iliyotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa msimu wa kilimo 2025/2026. Aidha, amesema TFC imeingiza tani 70,000 za mbolea aina ya NPK kwa ajili ya zao la tumbaku.

Kuhusu mahitaji ya mbolea katika msimu wa kilimo 2025/2026, alisema jumla ya tani milioni 1.5 zinahitajika, huku mwaka uliopita tani 962,000 zikitumika. Amesema tangu mwaka 2022 hadi sasa, serikali imetoa Sh bilioni 116 kama mtaji kwa TFC ili kuwezesha ununuzi wa mbolea ambayo huuzwa kwa bei ya ruzuku kwa wakulima waliosajiliwa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *