KATIKA wiki ya Kampeni ya Kifafa iliyofanyika Februari 5 hadi 9 mwaka huu, Chama cha Wataalamu wa Kifafa Tanzania (TEA) kilitangaza kuwa hatari ya wagonjwa wa kifafa kupoteza maisha imepungua nchini. TEA ilisema upungufu huo ni kutoka wastani wa vifo sita hadi nne, huku ikibainisha kuwa jitihada za utoaji elimu zimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza athari za ugonjwa huo.
Akizungumza Dar es Salaam, Daktari Bingwa wa Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu, Patience Njenje, alisema wanendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu kifafa na kuongeza mwamko wa wananchi kutafuta matibabu hospitalini. “Tunapongeza serikali kupitia Wizara ya Afya na wadau wengine wote kwa mapambano dhidi ya elimu potofu kuhusu kifafa, ambayo imechangia kupunguza vifo vya watu wengi waliokuwa wanaweza kupona au kupata nafuu kupitia tiba za hospitalini,” alisema Dk Njenje.
Amebainisha kuwa jamii, hususan katika maeneo ya vijijini, mara nyingi imedhani kuwa wagonjwa wa kifafa wamerogwa au kuwa ugonjwa unaambukiza, hali inayofifisha mikakati ya kukabiliana na kifafa. Kwa mfano, zaidi ya asilimia 36 ya jamii bado wanaamini kifafa kinatokana na nguvu za giza, na asilimia 50 wanaamini kuwa ni ugonjwa unaoambukiza.
Dk Njenje pia ametaja mchango wa mashirika ya kitaalamu kama TEA, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wadau kama POCET (Parents of Children with Epilepsy Tanzania) katika kukuza ufahamu na elimu kuhusu kifafa, jambo lililochangia mafanikio haya. Takwimu zinaonyesha kuwa vijana wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ndiyo kundi linaloongoza kupata kifafa, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ajali za pikipiki zinazoweza kuumiza sehemu za kichwa.
Amesema kuwa milo potofu imechangia Afrika kuwa na idadi kubwa ya watu wanaoishi na kifafa, kati ya watu 20 hadi 58 kwa kila 1,000, huku Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zenye wagonjwa wengi wa kifafa. Kwa mfano, vijiji vya Wilaya ya Mahenge vimetajwa kuwa na waathirika 37 kati ya watu 1,000. “Elimu inapaswa kuendelea kwa nguvu zote kuwafikia wananchi, kuondoa imani potofu na kuhakikisha idadi ya watu milioni 60 wanaoishi na kifafa duniani inapungua. Hii ni pamoja na kupunguza ongezeko la wagonjwa wapya kutoka watu 34 hadi 75 kwa kila watu 200,000 kwa mwaka,” alisema Dk Njenje.
Hata hivyo, alionya kuwa bado asilimia 60 ya vifo vinasababishwa moja kwa moja na kifafa, na zaidi ya asilimia 25 ya wagonjwa hupata ulemavu kutokana na kuanguka wakati wanapopata degedege. SOMA: “Wenye kifafa wasitengwe”
Dk Njenje amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kampeni za elimu kuhusu viashiria na sababu za kifafa, ikiwa ni pamoja na homa kali kipindi cha utotoni, minyoo ya nguruwe (hasa nyama isiyopikwa vizuri), uvimbe kwenye ubongo, na upungufu wa kinga mwilini. “Tushirikiane kutoa elimu hii ili kusaidia kumaliza kabisa ugonjwa huu nchini,” alisema.
