
Marekani imeitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kushughulikia ukatili unaofanywa dhidi ya raia, wakiwemo waasi wa AFC/M23, Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Masuala ya Afrika imetangaza siku ya Jumatano.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Vurugu zinazowalenga raia mashariki mwa DRC hazikubaliki, na tunahimiza pande zote kuheshimu usitishaji vita uliowekwa katika Azimio la Kanuni lililotiwa saini mjini Doha kati ya DRC na M23. (…) Tutaendelea kukuza uwajibikaji ili wale wanaohujumu amani, utulivu au usalama wawajibishwe,” Ofisi hiyo imesema katika taarifa yake.
Mpango huu unakuja huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakiongeza maonyo kuhusu hali hiyo. Katika ripoti iliyochapishwa siku ya Jumatano, Amnesty International imeshutumu dhuluma zinazofanywa na AFC/M23 na makundi yenye silaha ya Wazalendo yanayounga mkono serikali katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini: mauaji ya kikatili, ubakaji wa watu wengi, utekaji nyara dhidi ya wagonjwa, na mashambulizi hospitalini. Shirika hilo lisilo la kiserikali limeitaka Rwanda kubeba majukumu yake na kumtaka Rais Félix Tshisekedi kuwafungulia mashitaka wapiganaji wa Wazalendo wanaohusika na uhalifu huu.
Siku hiyo hiyo, Human Rights Watch imeshutumu AFC/M23 kwa kuwaua zaidi ya raia 140 mwezi Julai karibu na Mbuga ya Kitaifa ya Virunga, katika eneo la Rutshuru (Kivu Kaskazini), wengi wa waathirika wakiwa wakulima kutoka jamii ya Wahutu.
Kwenye uwanja wa vita, hali bado ni ya wasiwasi. Kulingana na vyanzo vya ndani vilivyonukuliwa na Actualité.cd, waasi wa AFC/M23 walianzisha ngome mpya siku ya Jumanne kati ya Kibati na Kaliki, katika eneo la Walikale, baada ya mapigano kadhaa na wanamgambo wa Wazalendo. Watu wameripotiwa kukimbilia katika vijiji jirani vya Kangati na Ngenge.
Ghasia hizi zinakuja chini ya miezi miwili baada ya kutiwa saini huko Washington mnamo Juni 27 kwa makubaliano ya amani kati ya DRC na Rwanda, ambayo yananuiwa kumaliza miongo kadhaa ya ukosefu wa utulivu katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.