
Polisi wanasema rais wa zamani wa Brazil Jair Bolsonaro aliandika barua ya kuomba hifadhi nchini Argentina huku uchunguzi kuhusu mapinduzi ya 2024 ukizidi.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Polisi wa Shirikisho la Brazil wamesema jumbe zilizopatikana kwenye simu ya mkononi ya rais wa zamani wa Brazil Jair Bolsonaro zinaonyesha kwamba wakati fulani alitaka kukimbilia Argentina na kutafuta hifadhi ya kisiasa kutoka kwa Rais wa Argentina Javier Milei.
Polisi wamesema katika ripoti iliyotolewa siku ya Jumatano kwamba barua hiyo ya hifadhi ilihifadhiwa kwenye simu ya Bolsonaro mnamo mwezi Februari 2024, siku chache baada ya pasipoti ya rais huyo wa zamani kukamatwa kama sehemu ya uchunguzi wa madai yake ya kuhusika katika njama ya mapinduzi.
Haijulikani ikiwa ombi hilo la hifadhi lilitumwa, na ofisi ya rais wa Argentina haijazungumza chochote kuhusiana na madai hayo.
Hati ya maombi ya hifadhi iliyotolewa siku ya Jumatano ilikuwa ni sehemu ya ripoti ya mwisho ya polisi ikimshtumu Bolsonaro na mtoto wake wa kiume, Eduardo, ambaye anaishi Marekani, kwa kuingilia mchakato wa kimahakama unaoendelea kuhusiana na kesi inayokuja ya rais huyo wa zamani kwa madai ya kupanga njama ya mapinduzi.
Kesi ya Bolsonaro imepangwa kuanza kusikilizwa Septemba 2. Anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 40 jela iwapo atapatikana na hatia ya kupanga kumpindua mrithi wake aliyechaguliwa kidemokrasia kama rais, Luiz Inacio Lula da Silva, mwaka wa 2022.
Polisi sasa wamependekeza kuwa rais huyo wa zamani na mwanawe wafunguliwe mashtaka ya “kulazimisha mchakato wa mahakama” na “kufuta sheria ya kidemokrasia” kuhusiana na kuingiliwa kwa mapinduzi. Hukumu ya pamoja ya makosa haya mawili inaweza kufikia miaka 12 jela.
Chombo cha habari cha Brazil O Dia kiliripoti siku ya Jumatano kwamba rekodi za sauti pia ziligunduliwa kwenye kifaa kilichokamatwa wakati wa uchunguzi wa polisi dhidi ya Bolsonaro. Rekodi hizi zilionyesha “majaribio ya kutisha mamlaka na kuzuia maendeleo ya uchunguzi kuhusiana na mashambulizi dhidi ya demokrasia, ikiwa ni pamoja na majaribio ya ushawishi kutoka nje.”
Bolsonaro, akiwa chini ya kifungo cha nyumbani tangu mapema mwezi Agosti, ameendelea kusema kuwa hana hatia wakati wa kesi ya mapinduzi, ambayo Rais wa Marekani Donald Trump, mshirika wake, ameiita “kesi ya kisian inayolenga kumuangamiza” rais hyuo wa zalani wa Brazil.
Mtoto wa Bolsonaro, Eduardo, alijiuzulu kama mbunge wa Brazil mwezi Machi na kuhamia Marekani, ambako anafanya kampeni kwa utawala wa Trump kuingilia kati kwa niaba ya baba yake.
Juhudi hizi za ushawishi zimefanikiwa, huku utawala wa Trump ukichukua hatua za adhabu dhidi ya Brazil katika kesi hiyo, ikiwa ni pamoja na vikwazo dhidi ya maafisa wa mahakama.
Trump pia aliweka ushuru mkubwa wa 50% kwa mauzo mengi ya Brazil kwenda Marekani, akitaja kesi ya Bolsonaro.