Mkataba huo, uliosainiwa mwaka 2010 kati ya Marekani na Urusi, uliweka ukomo wa idadi ya vichwa vya silaha za nyuklia, makombora na ndege za kimkakati kwa pande zote mbili. Kumalizika kwake kunamaanisha kuwa, kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka 50, hakuna tena vikwazo vya kisheria vinavyodhibiti silaha za nyuklia za mataifa hayo mawili yenye silaha nyingi zaidi duniani.
Akizungumza leo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Lin Jian, amesema kuwa mkataba wa New START ulikuwa na mchango mkubwa katika kulinda uthabiti wa kimkakati wa kimataifa. Amesema jumuiya ya kimataifa ina wasiwasi mkubwa kuwa kumalizika kwake kunaweza kuathiri vibaya mfumo wa udhibiti wa silaha na mpangilio wa kimataifa wa nyuklia.
China imezitaka Marekani na Urusi kuonyesha uwajibikaji, kujizuia, na kurejea haraka kwenye mazungumzo ya kimkakati. Beijing pia imeihimiza Washington kujibu kwa njia chanya pendekezo la Moscow la kuendelea kuheshimu kwa hiari mipaka ya msingi ya mkataba huo, ili kuzuia hali ya mashindano mapya ya silaha za kinyuklia.
”China inasikitikia kumalizika kwa Mkataba wa New START kati ya Marekani na Urusi. Mkataba huo una umuhimu mkubwa katika kudumisha uthabiti wa kimkakati wa dunia. Jumuiya ya kimataifa ina wasiwasi mkubwa kwamba kumalizika kwake kutakuwa na athari hasi kwa mfumo wa kimataifa wa udhibiti wa silaha na mpangilio wa nyuklia wa dunia.”
Kwa upande wake, Ikulu ya Urusi, Kremlin imesema inaona kumalizika kwa mkataba huo kama hatua hasi, lakini imeahidi kuendelea kuchukua msimamo wa uwajibikaji katika suala la uthabiti wa nyuklia. Rais wa Urusi, Vladimir Putin, alijadili suala hilo hivi karibuni na Rais wa China, Xi Jinping, katika mawasiliano ya ngazi ya juu kati ya nchi hizo mbili.
Marekani, kwa upande wake, imeeleza kuwa makubaliano yoyote mapya ya nyuklia yanapaswa kuijumuisha China. Hata hivyo, Beijing imesisitiza kuwa uwezo wake wa nyuklia hauko katika kiwango sawa na ule wa Marekani na Urusi, na hivyo China haitaingia katika mazungumzo ya kupunguza silaha za nyuklia kwa sasa. China, hata hivyo, imerudia msimamo wake wa kudumisha mkakati wa nyuklia wa kujilinda pekee.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameonya kuwa dunia inaingia katika hali isiyotabirika, bila mipaka yoyote ya kisheria inayodhibiti silaha za kimkakati za nyuklia.
Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye mara nyingi amekuwa akikosoa mipaka ya kimataifa inayowekewa Marekani, pia alionekana katika muhula wake wa kwanza kuwa tayari kuuacha Mkataba wa New START umalizike aliposisitiza kwamba China lazima ijumuishwe.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanasema kumalizika kwa mkataba huo kunatokana zaidi na namna utawala wa Trump ulivyofanya kazi kuliko misimamo ya kiitikadi, ambapo wanadiplomasia wa taaluma waliwekwa kando na kukosa uwezo na muda wa kujadiliana mkataba tata kama huo.