Katika Hospitali ya Al-Shifa huko Gaza, familia zimekusanyika kimya kimya huku zikiwa zimejaa huzuni, zikitafuta taarifa kuhusu wapendwa wao waliotoweka wakati wa vita.
Katika ukumbi uliotengwa kwa ajili ya utambuzi, picha za miili ya binadamu zinaoneshwa kupitia skrini. Wazazi, ndugu na jamaa wakiwa na sura za huzuni wanaangalia polepole kutoka picha moja hadi nyingine, wakitumaini lakini wakati huo huo kwa kuogopa kuwambua mpendwa wao.
Lori limefika likiwa limebeba mifuko myeupe ya plastiki 66 iliyojaa mabaki ya binadamu na sehemu za miili, yaliyowasilishwa kutoka Israel kwenda Ukanda wa Gaza. Wahudumu wa afya wanashusha mifuko hiyo kwa uangalifu na kuihamishia katika idara ya tiba ya uchunguzi wa maiti. Kwa familia nyingi zilizokuwa zikisubiri nje, hili lina uwezekano mchungu wa kupata majibu kuhusu ndugu zao waliopotea au kuongezeka kwa sintofahamu.
Mahmoud Adwan, Ndugu wa Mtu Aliyepotea akiwa amesimama mbele ya gari katika mazingira ya mjini Gaza. Nyuma yake ni watu wanaotafuta watu wao waliotoweka.
Umati wa watu umekusanyika katika lango la idara hiyo, wakiiuliza wahudumu taarifa yoyote kuhusu jamaa zao waliopotea. Allam Abu Wadi, ndugu wa mtu aliyepotea anaeleza akisema,
“Nilimpoteza kaka yangu akiwa bado mdogo. Alikimbilia kusini mwa Gaza wakati wa vita kutokana na hali ngumu iliyokuwa kaskazini mwa Gaza wakati huo. Alipopitia eneo la Nitsarim, alitoweka kabisa, na tangu wakati huo hatujapata habari zake. Tuliomba msaada kwa Msalaba Mwekundu na mashirika ya kibinadamu, lakini hakuna aliyeitikia. Leo, tunainua sauti zetu kwa ulimwengu; tunataka tu kujua watoto wetu walipotelea wapi.”
Ndani ya hospitali, friji za kuhifadhi maiti sasa zinahifadhi miili isiyotambuliwa. Timu za kitabibu zinafanya kazi chini ya shinikizo kubwa, zikijaribu kurekodi na kuhifadhi mabaki ili familia ziweze kupata majibu.
Ndugu na jamaa wanasema mchakato wenyewe ni wa kuumiza sana kisaikolojia, na unaongeza maumivu juu ya hasara ambayo tayari haihimiliki. Mahmoud Adwan, ambaye pia hajui ndugu yake yuko wapi na kama yuko hai au la analalamikia hali hii akisema, “miili haipaswi kuwasilishwa kwa namna hii ya kikatili. Sayansi imepiga hatua, na kuna njia mbadala nyingi zinazowezesha familia kutambua miili ya jamaa zao waliopotea, kama vile vipimo vya DNA yaani vinasaba au mbinu nyingine za kibinadamu. Njia hii haikubaliki. Familia hufika zikiwa katika hali dhaifu kisaikolojia; unawezaje kuuona mwili wa kaka yako ukiwa umeharibika bila taarifa yoyote na pengine usiweze hata kumtambua? Wengi watapatwa na mshtuko, na matokeo yake huenda wasiweze kuitambua miili hiyo.”
Wasiwasi wa kibinadamu unaendelea kuongezeka kutokana na kukosekana kwa vifaa vya kisasa vya kuwatambua marehemu, huku vikwazo vinavyoendelea kuhusu uingizaji wa mitambo mizito katika eneo hilo vikizidi kutatiza juhudi za kuwatafuta waliopotea.
Mamlaka za afya za Gaza zinasema zililazimika kuanzisha makaburi ya pamoja kwa miili isiyotambuliwa lakini zikiandikisha kila mwili kwa namba maalum kwa matumaini ya kuwatambua siku zijazo.