Rais wa Marekani, Donald Trump, alizua hasira katika duru za kisiasa baada ya kurusha mkanda wa video kwenye jukwaa lake la “Truth Social” akitangaza nadharia za njama za uchaguzi ikiwa na kile kilichoelezwa kuwa maudhui ya “ubaguzi wa rangi” yanayomuonyesha Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama na mkewe, Michelle kama nyani.

Kipande hicho cha video ya dakika moja, ambacho kiliondolewa mtandaoni baadaye, kinajumuisha madai ya mara kwa mara ya wizi wa kura katika uchaguzi wa 2020, kikiishutumu Dominion Voting Systems kwa kusaidia kuchakachua matokeo ya uchaguzi kwa niaba ya Wademokrati.

Video hiyo inaonyesha nyuso za Obama na mkewe, Michelle wakiwa kama nyani. Video hiyo ilikuwa imevutia zaidi ya watu elfu moja kwenye jukwaa hilo kufikia mapema jana Ijumaa, licha ya wimbi la ukosoaji mkali.

Gavana wa California, Gavin Newsom amelaani tukio hilo, huku ofisi yake ya vyombo vya habari ikielezea kitendo hicho katika ujumbe wake kwenye jukwaa la X kuwa ni “mwenendo wa kuchukiza kutoka kwa rais.” 

Ben Rhodes, afisa mkuu wa Baraza la Usalama wa Taifa katika utawala wa Obama, amesema, “Trump na wafuasi wake wanapaswa kuwa na wasiwasi kwamba Wamarekani wa siku zijazo wataiadhimisha familia ya Obama kama watu wapendwa, huku wakimuona Trump kama doa la aibu kwenye historia ya Marekani.”

Mtaalamu wa masuala ya kimkakati wa chama cha Democratic, Adam Parkhomenko, pia ameitaja video hiyo kuwa ni “ubaguzi wa rangi ulio wazi,” na kuongeza kuwa: “Huu ni ubaguzi wa rangi ambao hauwezi kufasiriwa vingine au kuhalalishwa, na hii ndio sura halisi ya Trump ambao tunaijua siku zote.”

Kwa upande mwingine, Rais wa Marekani, Donald Trump amesema hataomba msamaha kwa kurushwa hewani video hiyo, akisisitiza kwamba hakufanya kosa lolote.

Hata hivyo, baadaye, Ikulu ya White House ilitangaza kuwa inaondoa video hiyo yenye utata, ikisema kwamba mmoja wa wafanyakazi wake ameichapisha “kimakosa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *