Meneja wa timu ya Manchester City, Pep Guardiola aliisisitiza jana Ijumaa kwamba atapaza sauti yake waziwazi wakati wowote “watu wasio na hatia wanapouawa” popote pale duniani, akijibu ukosoaji wa Baraza la Wawakilishi wa Jumuiya ya Wayahudi la Jiji la Manchester nchini Uingereza.

“Kwa nini siruhusiwi kuelezea hisia zangu? Kwa sababu tu mimi ni kocha? Sikubaliani na jambo hilo, lakini naheshimu maoni yote,” amesema Guardiola katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya mechi ya Ligi Kuu ya England Jumapili ya kesho dhidi ya Liverpool.

Ameongeza kwamba: “Watu wasio na hatia wanauawa, na ninalaani vikali jambo hilo.”

Tamko hilo la Guardiola linakuja kujibu ukosoaji wa Bodi ya Wawakilishi wa Kiyahudi ya Greater Manchester kufuatia matamshi aliyotoa kabla ya mchezo wa pili wa nusu fainali ya Kombe la Carabao kati ya Manchester City na Newcastle Jumatano iliyopita.

Taarifa iliyotolewa na baraza hilo siku ya Alhamisi ilimtaka Guardiola “kuzingatia soka badala ya masuala ya kisiasa ya kimataifa.”

Guardiola amesema, inaumiza kushuhudia picha za raia wakiteseka licha ya maendeleo ya kisasa ya kiteknolojia na kijamii.

“Hatujawahi katika historia ya wanadamu kuwa na kila kitu waziwazi mbele ya macho yetu (kama hivi sasa),” alieleza kocha huyo wa Manchester City na kufafanua: “Mauaji ya kimbari huko Palestina, yaliyotokea Ukraine, Russia, Sudan – kila mahali. Hili ni tatizo letu kama wanadamu.”

Israel imeua maelfu ya watoto wa Kipalestina huko Gaza

“Si kuhusu Palestina pekee. Ni kuhusu kila piganio linaloweza kuufanya ubinadamu uwe na hali bora,” ameeleza Guardiola na kuendelea kubainisha: “watu wanaokimbia vita, wakiacha nchi zao, wakivuka Mediterania – usiulize kama ni sahihi au si sahihi (wanachofanya). Waokoeni. Wakati watu wanapokufa, inapasa uwasaidie”.

Huku akikosoa mauaji ya Renee Good na Alex Pretti yaliyofanywa na maafisa wa serikali kuu ya Marekani huko Minneapolis mwezi uliopita, Guardiola amesema matukio hayo yameonyesha kuwepo haja ya kupinga dhulma. “Tazama kilichotokea Marekani — Renee Good na Alex Pretti waliuawa,” amesema kocha huyo wa Man City, na kueleza bayana kwamba, vifo hivyo haviwezi kutetewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *