Kwa takriban miongo minane, kuanzia mwaka 1893 hadi 1960, Ivory Coast ilikuwa eneo la moja ya tawala za kikoloni katili zaidi za Ufaransa magharibi wa Afrika.

Kipindi hicho cha giza kiliambatana na uvamizi wa kijeshi, unyakuzi wa ardhi, mfumo wa kuwatumikisha watu kwa nguvu, ukandamizaji wa umwagaji damu dhidi ya kila aina ya mapambano na jitihada za kimfumo za kufuta utambulisho wa kiutamaduni wa wakazi asilia. 

Uwepo wa Ufaransa nchini Ivory Coast ambao ulianza kwa kutiwa saini mikataba ya upande mmoja na mara nyingi ya ulaghai na watawala wa ndani katika muongo wa 1840 ulipata msukumo mkubwa baada ya mkutano muhimu wa Berlin mwaka 1885. Katika mkutano huo, madola ya kikoloni ya Ulaya yalieleza kanuni kuu iliyopewa jina la “uvamizi wenye taathira” (effective occupation) kama mchezo mpya wa kuigawanya Afrika. Kwa mujibu wa kanuni hiyo, ilikuwa haitoshi kudai mamlaka ya eneo au nchi fulani kwa msingi wa mikataba michache ya pwani au uwepo wa kiishara tu; badala yake, kila nchi ya Ulaya ilipasa kuthibitisha uwepo wake halisi, wa kiutawala na kijeshi katika eneo husika. Kanuni hiyo iliibua mashindano ya kiendawazimu baina ya madola ya kikoloni kwa aliji ya kutwaa maeneo ya bara la Afrika na kuanzisha kambi za kijeshi na kiidara katika ardhi zilizavamiwa na kukaliwa kwa mabavu. 

Ili kufanikisha kanuni hiyo ya effective occupation, Ufaransa ilituma maafisa wake ndani ya ardhi hizo. Mmoja kati ya watu hao muhimu alikuwa Louis-Gustave Binger, afisa na mvumbuzi wa Ufaransa ambaye, wakati wa safari yake kubwa ya kiuvumbuzi kati ya mwaka 1887 hadi 1889 alieneza madai ya Ufaransa ya kumiliki maeneo mengi baada ya kusaini mikataba mingi na machifu wa maeneo mbalimbali nchini Ivory Coast. Aghalabu ya mikataba hiyo ilikuwa ikisainiwa katika hali na mazingira yya kutatanisha, kwa sababu machifu wengi hawakuwa na ufahamu sahihi kuhusu sheria iliyoandikwa ya kukabidhi mamlaka ya maeneo yao kwa utawala wa kikoloni. Kwa msingi huo, mikataba yote iliyokuwa na utata na iliytoegemea mantiki ya kanuni ya “effective occupation”  hatimaye iliiwezesha Ufaransa Machi 10, 1893  kuitambua rasmi Ivory Coast kama koloni lake, na Binger akateuliwa kuwa gavana wa kwanza wa utawala wa kikoloni wa Paris nchini humo. Siku hiyo iliashiria kuanza rasmi utawala wa moja kwa moja kikoloni wa Ufaransa nchini humo. 

Kabla ya kufika Ivory Coast, Ufaransa ilikuwa imejaribu mtindo wa utawala wake wa kikoloni katika baadhi ya makoloni yake mengine kama vile Algeria, na ilikuwa imejifunza jinsi ya kupora ardhi zenye rutuba za wenyeji na kuzikabidhi kwa wahamiaji wa Ulaya (wakoloni) kupitia ukandamizaji wa umwagaji damu dhidi ya mapambano na harakati za ukombozi za wananchi. 

Wakati Ufaransa iliposimika utawala wake wa kikoloni nchini Ivory Coast, misingi ya utawala huoilikuwa na mihimili miwili mikuu: Mosi, sera ya unyakuzi wa ardhi na kubadilisha jamii ya watu  kiasi kwamba ardhi ya pamoja ya jamii na kilimo cha wenyeji hasa ardhi za watu wa kabila la Baoulé ziliporwa kwa anwani ya “ardhi zisizo na wamiliki” na kukabidhiwa kwa wakoloni wa Kifaransa kwa ajili ya kuanzisha mashamba makubwa ya kakao, zao la kahawa na kilimo cha ndizi. 

Pili na muhimu zaidi, ilikuwa utekelezaji wa “Pili na muhimu zaidi ilikuwa utekelezaji wa “Sheria Maalumu kwa Ajili ya Wenyeji” au “Indigenous Code”. Sheria hiyo ambayo ilionekana kuwa wenzo mkuu wa udhibiti na kutia hofu, iliwaarifisha wenyeji kuwa watu duni na wasio na haki. Kwa mujibu wa sheria hiyo, kila raia mwenyeji aliadhibiwa kwa mujibu wa uamuzi wa afisa wa utawala wa kikoloni bila ya kufunguliwa mashtaka. Mara nyingi, tuhuma zilizotolewa hazikuwa zikieleweka au kuwa wazi kama vile “kumvunjia heshima afisa wa Ufaransa,” “kuvuruga nidhamu ya umma” au hata “kuwa na mtazamo usiofaa.” Adhabu za haraka na kali za kanuni hiyo zilijumisha kuchapwa viboko, vifungo virefu gerezani, faini nzito za pesa na kupelekwa kwenye kambi za kazi ngumu. Ni wazi kuwa, sheria hizo maalumu kwa wenyeji ulikuwa mfumo wa sheria ambayo ulihalalisha ukatili wa za kila siku na wa kimfumo wa utawala wa kikoloni wa Ufaransa, na kuzima mapambano ya kila aina au upinzani uliokuwa ukijitokeza dhidi ya wakaloni hao.

Kigezo cha utawala wa ukoloni wa Ufaransa huko magharibi mwa Afrika kilibuniwa kwa lengo la kuanzisha utaratibu wa utiifu kamili kwa watawala wa kikoloni. Hata hivyo utaratibu huo wa kulazimisha kamwe haukukubaliwa kirahisi. Mapambano ya ukombozi dhidi ya uvamizi wa Ufaransa yalikuwa sehemu isiyoweza kutenganishwa na historia ya zama hizo. 

Changamoto kubwa na iliyopangwa vizuri zaidi kwa sera ya kujitanua ya Ufaransa huko Magharibi mwa Afrika ilikuwa utawala wa Kiislamu uliokuwa na nguvu ulioanzishwa na Samory Touré  katika sehemu kubwa ya Afrika Magharibi. Jeshi lake lililopangwa vizuri na lililokuwa na zana za kutosha, ambalo lilikuwa na uwezo wa kutengeneza silaha za moto, lilikuwa kizuizi kikubwa katika njia ya kusonga mbele Wafaransa kwa miaka mingi. Kutokana na ukweli kwamba mapigano ya moja kwa moja na kikosi cha utawala huo yalikuwa wa gharama kubwa kwa Ufaransa, jeshi la utawala wa kikoloni la Ufaransa lilitumia mbinu za kikatili zaidi kadiri iwezekanavyo ikiwa ni pamoja na sera ya ardhi iliyoteketea (scorched earth policy). Wanajeshi wa Ufaransa waliharibu vijiji kwa makusudi, walichoma mashamba na maghala ya chakula, na kuchafua vyanzo vya maji kwa sumu ili kuzuia msaada wowote wa wananchi kwa utawala wa Kiislamu wa Touré. Vitendo hivyo vilivyofanyika kwa mahesabu maalumuu na ukatili wa kutisha, vilisababisha njaa kali ya makusudi ambayo ilisababisha vifo vya maelfu ya raia wasio na hatia waliopoteza maisha kutokana na njaa na magonjwa.

Wafaransa walikandamiza mapambano yote ya ukombozi barani Afrika

Hatimaye, mnamo 1898, Samory Touré alikamatwa na kupelekwa uhamishoni, lakini huo haukuwa mwisho wa mapambano. Upinzani wa Waafrika wenyeji uliendelea katika aina zingine, haswa kutoka kwa jamii kama vile watu wa Baoulé ambao hawakuwa tayari kuachia ardhi zao zenye rutuba kwa walowezi na wakoloni wa Kifaransa.

Kiini cha unyonyaji wa kiuchumi wa utawala wa kikoloni wa Ufaransa kilitegemea mfumo wa kazi za kulazimishwa. Kila mtu mzima mwanaume alilazimika kufanya kazi siku 10 hadi 15 kwa mwaka bila malipo katika miradi ya serikali ya kikoloni kama vile ujenzi wa barabara, njia za reli kama ile ya Abidjan-Niger, na majengo ya ofisi za utawala. Mazingira ya kambi hizo za kazi za kulazimishwa yalitawaliwa na utapiamlo, magonjwa yaliyoenea, na sulubu, na kiwango cha vifo miongoni mwa wafanyakazi hao Waafrika kilikuwa cha juu. Zaidi ya hayo, kila mwanaume aliiyebalehe alilazimishwa kutoa kodi ya kichwa. Lakini kwa kuwa uchumi wa pesa haukuwa umeenea katika maeneo mengi ya Afrika, wenyeji walilazimishwa kufanya kazi kwa makampuni ya kikoloni au mashamba ya wakoloni ili kulipa kodi hiyo, ambayo iliunda aina nyingine ya kazi ya kulazimishwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *