Marekani inajaribu kudumisha nafasi yake barani Afrika kupitia matumizi ya mabavu na ghiliba za kisiasa, huku ikizingatia zaidi nishati na madini muhimu, tofauti na ushirikiano mpana wa kiuchumi wa China katika bara hilo.

Hayo yamesema na Andrey Maslov, mkuu wa Kituo cha Tafiti za Afrika katika Chuo Kikuu cha Uchumi cha Moscow katika mahojiano na RT ambapo amesifu uamuzi wa China kuondoa ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi 53 za Afrika. Hatua hiyo, inayotarajiwa kuanza kutekelezwa tarehe 1 Mei, ilitangazwa na Rais wa China, Xi Jinping, katika ujumbe wake kwa Umoja wa Afrika (AU) wakati wa mkutano wa kilele uliofanyika nchini Ethiopia.

Kwa mujibu wa maafisa, sera hiyo ya ushuru wa sifuri inalenga kuimarisha biashara kati ya China na bara la Afrika. Maslov amesema hatua hiyo inaakisi juhudi za Beijing za kuelekeza upya mwelekeo wa biashara yake ya kimataifa.

Aidha amesema kuwa, kupungua kwa idadi ya watu na kuongezeka kwa gharama za kazi, kunazihamasisha kampuni nyingi za China kuhamishia uzalishaji wao nje ya nchi, ikiwemo barani Afrika.

Hatua ya China inakuja katika kipindi ambacho mvutano wa kibiashara kati ya Washington na baadhi ya nchi za Afrika unaongezeka, zikiwemo Afrika Kusini, ambayo imekabiliwa na shinikizo la ushuru na migogoro ya kibiashara na kidiplomasia na Marekani.

Kwa mujibu wa Maslov, lengo kuu la Washington katika kutoza ushuru kwa bidhaa za Afrika linatokana na kile alichokiita “mgogoro wa ndani wa Marekani yenyewe.” Ameongeza kuwa Marekani imelazimishwa kuingia katika mkondo wa kujitenga (isolationism).

Maslov amesema kuwa Marekani kwa muda mrefu imenunua uongozi wa dunia kwa gharama ya kuwalinda wazalishaji wake wa ndani, lakini sasa haiwezi tena kumudu hali hiyo.

China imekuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa Afrika kwa karibu miongo miwili, ikifadhili miradi ya reli nchini Kenya, maeneo ya viwanda nchini Ethiopia, pamoja na miradi ya uchimbaji madini nchini Zambia, huku ikiendelea kuimarisha uhusiano wake wa kibiashara na kiuchumi katika bara lote la Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *