
Dar es Salaam. Hivi umewahi kuingia kwenye mtandao wa Instagram, Facebook, X au Tiktok ukakutana na video au picha ukaanza kujiuliza kama ni halisi au imetengenezwa na akili unde (AI)?
Kama umewahi basi hiyo ndiyo hali halisi ya sasa baada ya kuibuka kwa kasi kwa AI katika utengenezaji wa picha na video, ambapo kumeanza kuacha alama kubwa katika tasnia ya habari na mawasiliano.
Leo, maudhui yanaposambaa mtandaoni, watu hawakimbilii tena kuyaamini badala yake hujiuliza kupitia sehemu ya kuandika maoni kwamba je, hii ni halisi au ni kazi ya AI?”
Hali hiyo imechochewa na kuongezeka kwa matumizi ya deepfakes yaani video au picha zinazoweza kumwonesha mtu akisema au kufanya jambo ambalo hakuwahi kulifanya. Tafiti mbalimbali zinaonesha changamoto hii si ya kinadharia, bali ni halisi na ina athari pana kwa jamii.
Profesa Hany Farid wa Chuo Kikuu Berkeley, California, ambaye ni mtaalamu wa uchunguzi wa picha za kidijitali, ameonya mara kadhaa kupitia tafiti zake kuwa macho ya binadamu hayatoshi tena kutambua udanganyifu wa sasa wa picha na video za AI.
Anasisitiza umuhimu wa kuwekeza katika teknolojia za kuthibitisha uhalisia wa maudhui (content authentication tools).
Akizungumza na Mwananchi, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura anasema kabla ya AI kwanza imani ya watu ilishapungua juu ya vyombo vya habari, ndio maana vimekuwa vikijaribu kuomba kurudi kwa umma.
“Kuhusu AI ni nzuri na ni mbaya, inapaswa tuitumie vizuri, ipo kutusaidia kazi zetu tunapaswa kuitumia kufichua maovu ndipo imani ya umma itarudi na kuongezeka.”
Anasema kusipochukuliwa hatua katika miaka ijayo hali itakuwa mbaya zaidi, akifafanua vyombo vya habari vinapaswa kutumia ‘fact checks techniques’, kutoa taarifa za uharaka kuhusu uhalisia, vivyo hivyo kwa waandishi waendane na teknolojia ili umma ujue ukweli wa maudhui hayo.
Ripoti ya kila mwaka ya Reuters Institute for the Study of Journalism imekuwa ikionesha kupungua kwa viwango vya imani ya umma kwa habari katika nchi nyingi.
Pia, Ripoti ya Digital News inaeleza kuwa hofu ya taarifa potofu na maudhui yanayotengenezwa kwa AI ni miongoni mwa sababu zinazochangia kushuka kwa imani hiyo.
Ripoti ya mwaka 2023 ya World Economic Forum pia imeiweka taarifa potofu inayochochewa na AI miongoni mwa hatari kubwa kwa uthabiti wa kijamii na kisiasa, ikieleza kuwa inaweza kudhoofisha imani kwa taasisi, mifumo ya uchaguzi na vyombo vya habari.
Watafiti wa Chuo Kikuu Stanford katika tafiti za saikolojia ya taarifa wamebaini kuwa kadiri watu wanavyozidi kukutana na maudhui ya kupotosha, ndivyo wanavyojenga tabia ya kutilia shaka kila kitu wanachokiona mtandaoni hata kama ni sahihi.
Hali hii hufanya hadhira kuamua kujiondoa au kupunguza imani kwa vyanzo vyote wanavyoviona. Athari zake zinaanza kuonekana hata katika matukio ya kijamii na kisiasa, ambapo baadhi ya watu wanaweza kukataa ushahidi halisi kwa kudai ni matokeo ya AI.
Mtumiaji wa mitandao ya kijamii kutoka jijini Dar es Salaam, Mathew Sebastian anasema sababu ya kupungua kwa imani ya vitu vinayowekwa mitandaoni hasa vikihusisha picha na video ni AI ambayo imekua kwa kasi sana.
“Sasa kuna zana zinazoweza kutengeneza picha na video zenye ubora mkubwa kiasi kwamba zinafanana kabisa na halisi. Watu wengi pia wanazitumia kwa ajili ya kutafuta wanaofungua kuangalia kazi zao na kufuatiliwa. Kabla sijatoa maoni lazima niangalie chanzo cha post au source kama imetoka kwenye ukurasa unaoaminika au laa,’’ amesema.
Mariam Ramadhan anasema bado inamuwia vigumu kutofautisha AI na uhalisia akisema anahitaji apate darasa ili asiwe anatoa maoni ya uhalisia kwenye maudhui feki.
Kwa wachambuzi wa mawasiliano, suluhisho si kupiga marufuku AI, bali kuimarisha mifumo ya uthibitishaji wa maudhui, kuweka alama za kidijitali (watermarks) na kuwekeza katika elimu ya uelewa.
Kadiri AI inavyoendelea kuwa sehemu ya maisha ya kila siku, swali linalobaki ni moja je, jamii itaweza kuendana na kasi ya teknolojia bila kupoteza imani kwa kile inachokiona na kukisikia?
Noel Henjewele Mkuu wa kitengo cha AI na Cloud kutoka Dynatech Solutions Limited anasema AI haikimbiliki bali kilichopo ni kuweza kuishi nayo na kwa namna yeyote lazima kuwe na misingi ya kuitumia.
“Kuhusu sekta ya habari suala hili lipo na maudhui yanayotengenezwa pia ni changamoto cha kufanya ni watu kupata elimu ya utambuzi ni maudhui ya AI au halisi. Elimu ndiyo inahitajika kwa sasa,” amesema.