Dar es Salaam. Kila ifikapo Machi 8, dunia huadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kutambua mchango wa wanawake katika nyanja mbalimbali za maisha.
Lakini ndani ya kuta za Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), maadhimisho haya yana tafsiri ya kipekee ya ujasiri, huruma na mapambano ya kila siku ya kuokoa maisha.
Hapa, muuguzi mwanamke mwenye uzoefu wa miaka 41, Febronia Kauki amekuwa mstari wa mbele si tu katika kutoa huduma za kitabibu, bali pia katika kuimarisha matumaini ya wagonjwa wanaokabiliwa na saratani.
Katika mahojiano maalumu kuelekea Siku ya Wanawake Duniani na Mwananchi, muuguzi huyu anasimulia safari yake, changamoto za kazi yenye uzito wa kihisia na namna alivyogeuza taaluma yake kuwa mwanga wa faraja kwa mamia ya wagonjwa na familia zao.
Novemba 1984, akiwa kijana mwenye ndoto na moyo wa kuhudumia, Febronia alianza kazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kama nesi muuguzi.
Hakujua kwamba safari yake ingetengeneza historia binafsi ya miaka karibu minne ya kuhudumia wagonjwa wa saratani na kushuhudia mabadiliko makubwa ya sekta ya afya nchini.
“Enzi zile ukifanya kazi kwa bidii na weledi, unapandishwa cheo,” anakumbuka kwa tabasamu la upole.
Ndani ya miaka mitatu, alipanda hadi kuwa muuguzi msaidizi. Wakati huo walivaa gwanda la kijani, baadaye wakabadilika na kuvaa sare nyeupe kama alama ya majukumu mapya na nidhamu ya kazi.
Mwaka 1988, alihamishiwa Ocean Road, iliyokuwa bado chini ya Muhimbili. Anasimulia kuwa kwa wakati huo wauguzi walikuwa wakibadilishana vituo kati Muhimbili na Ocean Road.
Lakini uhamisho huo haukuwa wa kawaida, alitoka na kwenda kuyaanza maisha mapya aliyoishi kwa miaka 38 akishuhudia mabadiliko ngazi kwa ngazi, ukuaji wa teknolojia ya matibabu ya saratani na ongezeko la vifaa na wataalamu.
Anasema siku za mwanzo aliogopa. Eneo la Upanga lilikuwa na msitu mzito, na hospitali ilikuwa mbali. Wauguzi walikutana Posta na kutembea kwa makundi hadi hospitalini kwa hofu ya usalama. “Haikuwa rahisi kutembea peke yako,” anasimulia.
Ndani ya wodi, hali ilikuwa ngumu zaidi
Wagonjwa wengi walifika katika hatua za juu za ugonjwa. Wengine hawakujua hata Kiswahili akiwa muuguzi ilimbidi afanye kazi ya ziada kuwasiliana nao.
Utambuzi wa mapema haukuwepo. Vidonda vilikuwa vikubwa, vingine vinatoa usaha au damu nyingi. Wengine walifika wakiwa na maumivu makali kupita kiasi.
“Nakumbuka siku yangu ya kwanza kazini alifika mama mmoja na nilimuona akitokwa damu nyingi ukeni. Ilitushangaza, lakini tulishirikiana na madaktari kupambana kuokoa maisha yake,” anasema.
Kutoka mapokezi ya ajali Muhimbili, alikokuwa akishughulika na wagonjwa waliokaa muda mfupi kabla ya kuruhusiwa, Ocean Road ilikuwa dunia nyingine.
Muuguzi katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Febronia Kauki
Hapa, wagonjwa walikaa muda mrefu kwa matibabu ya saratani. Wakati huo, taasisi hiyo ndiyo ilikuwa kituo kikuu cha saratani nchini, ikipokea wagonjwa kutoka mikoa yote.
Febronia mama wa makamo anayetarajia kustaafu Julai Mosi, mwaka huu anasimulia kuwa katika kipindi chake cha kufanya kazi kulikuwa na nyakati za majonzi na huruma isiyoelezeka.
Anakumbuka mgonjwa kutoka Kahama aliyegundulika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi baada ya kujifungua. Alikuwa na mtoto mchanga na hakuwa na msaada wa karibu. “Tulikuwa tunambeba yule mtoto, mama akiwa kwenye mionzi tunamnywesha uji na kumlea kwa zamu,” anasema kwa sauti ya kumbukumbu nzito.
Kwa Febronia, kazi ya uuguzi haikuwa tu kutoa dawa. Ilikuwa ni tiba ya mwili na moyo, “Wagonjwa wakisikia wana saratani wanaamini ndiyo mwisho wa maisha yao. Inabidi ukae nao, uwaeleweshe kwamba watapata matibabu na wanaweza kupona.”
Hayo yalikuwa maisha yake kwa kipindi chote cha miaka 38, wagonjwa wapya wakiingia katika hospitali hiyo, kupata matibabu na kuondoka na asilimia kubwa wakilazwa.
Anasema saratani ya matiti na shingo ya kizazi zilikuwa zikileta changamoto za kijamii pia. Kwa kipindi hicho ameshuhudia baadhi ya wanawake wakitengwa na familia, hata kuachwa na waume zao.
“Inaumiza sana kuona mwanamke anapopata ugonjwa, mwenza wake anamkimbia. Tumekua tunawasaidia kisaikolojia na kuwapeleka wengine ustawi wa jamii pale inapohitajika.”
Kulikuwa pia na hofu ya maambukizi ya Ukimwi miaka ya 1980 hadi mwaka 2000 jambo lililowalazimu kuwa waangalifu zaidi wanapohudumia wagonjwa, lakini bila unyanyapaa.
Miaka ilivyoenda, Febronia ameona mabadiliko makubwa.
“Mwanzo tulikuwa na na mashine moja tu ya kutibu saratani. Leo tuna mashine nyingi za kisasa.” Anataja kuongezwa kwa mashine ya pili, baadaye Linear Accelerator (Linac), na sasa kufungwa kwa PET-CT Scan hatua zinazorahisisha uchunguzi na matibabu ya haraka.
Febronia muuguzi mcheshi anayefanya kazi wodi ya mionzi ya ndani hospitali hapo, anasema tofauti na zamani, wagonjwa sasa wanakuja mapema zaidi. Uelewa umeongezeka. Wengi wanajua kuwa saratani ikigundulika mapema inatibika.
“Zamani walikuwa wanaogopa hata kuja kuchoma mionzi. Sasa wanafahamu na wanakuja kwa wakati.”
Hata mazingira ya kazi yameimarika. Anakumbuka enzi ambazo hospitali haikuwa na uzio, zamu za usiku zilikuwa changamoto na waliweza kufanya kazi za usiku kwa siku saba mfululizo bila malipo ya ziada. Maboresho yalipofanyika, walihisi kuthaminiwa.
Kwa miaka 38 Ocean Road, Febronia amejifunza kugawa muda kati ya kazi na familia. Alifanya kazi hadi saa nane mchana, kisha kurudi nyumbani kutekeleza majukumu ya kifamilia kama mama.
“Kazi imenifundisha kuthamini muda, kufanya kazi kwa bidii na kuwa na upendo kwa wagonjwa na jamii.”
Leo, tamanio lake ni kuona wauguzi wa saratani wakiboreshwa masilahi na kupewa nafasi zaidi za kuongeza ujuzi. “Tukiwezeshwa zaidi, tutahudumia kwa weledi mkubwa zaidi.”
Kwa wanawake, ana ujumbe mmoja wa dhati, wajitokeze kupima afya mara kwa mara, hasa saratani ya mlango wa kizazi. “Ikigundulika mapema, inatibika.”
Muuguzi katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Febronia Kauki
Anahitimisha kwa shukrani kwa uongozi wa nchi kwa maboresho ya sekta ya afya, akisema huduma zimeimarika na vifaa vimeongezeka, wagonjwa wanapata matibabu kwa wakati.
Lakini zaidi ya mashine na majengo, hadithi ya Febronia ni ya moyo. Moyo wa muuguzi aliyeona maumivu makubwa, aliyebeba watoto wa wagonjwa, aliyefuta machozi ya waliokataliwa, na aliyeshuhudia safari ya Taifa kutoka sindano za kuchemsha hadi teknolojia ya kisasa. Ni simulizi ya huduma, huruma na matumaini.