Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa amesema hatua za kijeshi zinazochukuliwa na Israel huko Ghaza si suala tena la kujilinda na zinaonekana kuwa na lengo la kuufanya uundaji wa nchi ya Palestina hapo baadaye usiwezekane.

Costa ameyasema hayo katika mahojiano na jarida la Le Grand Continent siku ya Jumatatu, na kusisitiza kwamba Israel lazima ikubali kusitishwa mapigano, iruhusu misaada ya kibinadamu kuingizwa Ghaza, na kusitisha ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

“Tangu mwanzo, tuliitambua haki ya Israel ya kujilinda, ikiwa ni pamoja na nje ya mipaka yake. Hata hivyo, ni wazi sasa kwamba hatua za kijeshi za Israel hazina tena maana ya kujilinda,” ameeleza rais huyo wa Baraza la Umoja wa Ulaya.

“Hakuna maneno yanayoweza kuelezea maafa ya kibinadamu yanayotokea Ghaza. Kutumia njaa kama silaha ya vita haikubaliki … Lengo la Israel ni kudhoofisha uhai wa nchi ya Palestina,” ameongezea kusema Costa.

Katika mahojiano hayo, Rais wa Baraza la Ulaya ametilia shaka pia lengo lililotajwa na Israel la kuanzisha vita dhidi ya Ghaza la kuiangamiza Hamas, akisema kundi hilo limezatiti uwezo wake licha ya miaka miwili ya mzozo huo mkubwa wa vita.

“Kuna uwezekano wa kuwepo hali mbili katika suala hili: ama operesheni hiyo haikufaulu kwa sababu imeshindwa kuiangamiza Hamas, au lengo halisi lilikuwa ni jambo lingine. Ni la kuiteketeza Ghaza ili kulifanya suala la Wapalestina kuishi kwa amani katika nchi yenye mamlaka ya kujitawala lisiwezekane”, ameeleza mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa EU.

Tangu Oktoba 7, 2023 hadi sasa, utawala wa kizayuni wa Israel umekuwa ukiendesha vita vya kinyama na mauaji ya kimbari huko Ghaza, ambayo hadi sasa yameshateketeza roho za Wapalestina zaidi ya 65,000 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Vita hivyo vimesababisha pia mamia ya maelfu ya watu walazimike kuyahama makazi yao pamoja na kuzuia misaada ya kibinadamu ambako kumegharimu maisha ya Wapalestina 442 wakiwemo watoto 147…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *