
Dar es Salaam. Tiba za asili zimeendelea kuwa nguzo muhimu ya huduma za afya nchini Tanzania, huku Ripoti ya Ukaguzi wa Utendaji ya mwaka 2024 kuhusu Udhibiti wa Tiba za Asili na Mbadala ikikadiria kuwa kati ya asilimia 60 hadi 80 ya wananchi hutegemea tiba hizo kwa mahitaji yao ya msingi ya afya.
Katika Jiji la Dar es Salaam, sekta hii imekua kwa kasi, hasa katika maeneo ya Kariakoo, Mbagala, Buguruni na Manzese, ambayo yameibuka kuwa vitovu vikuu vya biashara na usambazaji wa dawa za asili.
Hata hivyo, ukuaji huo wa haraka mijini umekwenda kasi kuliko uwezo wa udhibiti wa mamlaka husika, hali ambayo wataalamu wanasema imewaweka watumiaji katika hatari kubwa za kiafya ambazo zingeweza kuzuilika.
Madaktari jijini wanasema wanazidi kukutana na wagonjwa wenye madhara yanayohusishwa na matumizi ya dawa za asili zisizothibitishwa.
Kwa upande wake, daktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Dk Agnes Kweka, anasema wagonjwa wengi hufika hospitalini wakiwa katika hali mbaya baada ya kutumia tiba za mitishamba.
“Wagonjwa wengi huja wakiwa na matatizo yaliyozidishwa na matumizi ya dawa za asili. Baadhi ya dawa hizo, hasa zinapotumika sambamba na tiba za kisasa, zinaweza kusababisha hatari kubwa,” anasema.
Akiunga mkono hoja hiyo, mfamasia na mtafiti wa tiba za kitabibu jijini Dar es Salaam, Dk Clemence Mushi, anasema imani ya umma kwa tiba za asili imekua kwa kasi kuliko uelewa wa masuala ya usalama.
“Watumiaji wengi hudhani kuwa kila duka ni salama. Ukweli ni kwamba baadhi ya bidhaa zinaweza kuwa na viambata hatari, dozi zisizo sahihi au uchafuzi. Uhamasishaji na ufuatiliaji ni muhimu kulinda afya ya umma,” amesema.
Kiini cha tatizo kiko katika mnyororo mpana lakini usio rasmi wa usambazaji. Malighafi zinazoingia katika soko la Dar es Salaam hutoka katika mikoa kama Morogoro, Arusha, Manyara na Zanzibar, maeneo yenye utajiri wa bioanuwai na historia ndefu ya matumizi ya mitishamba.
Baada ya kuvunwa, malighafi hizo hupitia mitandao isiyo rasmi ya wasafirishaji, wauzaji wa jumla, wasindikaji na wauzaji wa rejareja kabla ya kuwafikia watumiaji kupitia maduka ya kawaida au majukwaa ya mtandaoni yanayoendeshwa na mawakala wasio rasmi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2024, kati ya bidhaa 499 za tiba za asili zilizochukuliwa sampuli Dar es Salaam, ni nane pekee zilikuwa zimesajiliwa rasmi, jambo linaloonesha pengo kubwa kati ya sera na utekelezaji.
Wataalamu wanasema pengo hilo linachangiwa pia na udhaifu wa usimamizi wa kidijitali. Shughuli za tiba za asili bado hazijaunganishwa kikamilifu katika mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa afya (AfyaSS), hali inayozuia mamlaka za udhibiti kufuatilia kwa wakati halisi wataalamu, bidhaa au madhara yanayoripotiwa.
Wakati huohuo, changamoto za kifedha zinaendelea kudhoofisha juhudi za utekelezaji wa sheria. Kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2025, fedha zilizotengwa kwa ajili ya udhibiti wa tiba za asili na mbadala zilishuka kutoka Sh2 bilioni katika mwaka wa fedha 2023/24 hadi Sh329 milioni katika mwaka 2024/25.
Daktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk Asha Suleiman, anasema upungufu huo umeathiri moja kwa moja uwezo wa mamlaka kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa mara kwa mara.
“Udhibiti unahitaji rasilimali watu, usafiri na msaada wa maabara. Bila fedha za kutosha, utekelezaji hubaki wa kinadharia badala ya kuwa wa vitendo,” anasema.
Mbali na udhaifu wa taasisi, wataalamu wanasema imani ya muda mrefu ya jamii kwa tiba za asili pia inafanya udhibiti kuwa changamoto. Wakazi wengi wa Dar es Salaam huendelea kuzitegemea kwa sababu ya mazoea ya kitamaduni na uzoefu wa familia na jamii, ambako matokeo chanya huimarisha dhana ya usalama.
Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa imani ya kitamaduni haiwezi kuchukua nafasi ya uthibitisho wa kisayansi.
Daktari na mtaalamu wa afya ya umma, Dk Neema Kessy, anasema kukosekana kwa mifumo rasmi ya rufaa na kuripoti kumeruhusu vitendo hatarishi kuendelea bila kugundulika.
“Mfumo wa rufaa uliopangwa vizuri huhakikisha wagonjwa wenye hali ngumu wanaelekezwa hospitalini, huku athari za dawa za asili zikirekodiwa na kuchambuliwa kitaalamu,” amefafanua.
Kwa msisitizo juu ya usimamizi wa kisayansi, mtafiti wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dk Benson Mugaka, anasema ukuaji wa kibiashara wa sekta haujaambatana na udhibiti wa ubora.
“Kila dawa lazima ipitie utambuzi wa kibotania, uchambuzi wa kemikali na upimaji wa dozi. Ukuaji wa haraka bila tahadhari hizi huweka watumiaji katika hatari ya sumu, metali nzito na uharibifu wa viungo vya mwili,” anasema.
Wataalamu pia wanasema hatari hazianzi kwenye eneo la mauzo pekee. Utegemezi wa mimea inayovunwa porini huongeza uwezekano wa uchafuzi, kutokuwepo kwa viwango thabiti vya nguvu ya dawa na hata uharibifu wa mazingira.
Daktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala, Dk Emmanuel Nyankunga, anaonya kuwa uzembe katika hatua yoyote ya mnyororo unaweza kuhatarisha usalama wa wagonjwa.
“Kuanzia uvunaji, usindikaji hadi uhifadhi, utunzaji usiofaa unaweza kuingiza uchafuzi. Ufuatiliaji wa mnyororo na viwango sahihi ni muhimu kulinda wagonjwa,” anasema.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, wataalamu wanasema udhibiti unapaswa kubadilika kutoka hatua za kuzima moto hadi mfumo jumuishi wa kinga na ufuatiliaji.
Hatua muhimu ni kuwaunganisha kikamilifu waganga wa tiba za asili na maduka yao katika mfumo wa AfyaSS. Hii itasaidia mamlaka kufuatilia maduka yaliyosajiliwa kwa wakati halisi, kubaini bidhaa zisizosajiliwa na kupanga ukaguzi kwa ufanisi zaidi, hasa katika maeneo yenye msongamano mkubwa kama Kariakoo na Mbagala.
Aidha, wataalamu wanasisitiza umuhimu wa fedha za kutosha na za kudumu ili kurejesha ukaguzi wa mara kwa mara na shughuli za uhamasishaji.
Dk Kweka anasema bila usimamizi endelevu, vitendo visivyozingatia sheria vitaendelea.
“Ufuatiliaji unahitaji wataalamu, usafiri na vifaa. Vitu hivyo vikikosekana, udhibiti hupoteza maana,” anasema.
Ujenzi wa uwezo pia umetajwa kuwa muhimu. MUHAS tayari imeanzisha mafunzo ya muda mfupi kwa wazalishaji na wauzaji wa dawa za asili, yakilenga Kanuni Bora za Utengenezaji (GMP), uzingatiaji wa sheria, usajili wa bidhaa, ufungashaji salama na viwango vya ubora.
Dk Mugaka anasema kuongeza uelewa wa kiufundi katika mnyororo mzima ni hatua muhimu ya kupunguza hatari.
“Mafunzo yanawasaidia wahusika kuelewa taratibu za usalama na madhara ya kutokuzifuata. Hii inalinda watumiaji na kuimarisha imani katika sekta,” anasema.
Wataalamu pia wanasisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano kati ya tiba za asili na huduma za kisasa za afya kupitia mifumo rasmi ya rufaa na ukusanyaji wa takwimu za madhara.
Dk Kessy anasema bila kumbukumbu sahihi, madhara hubaki simulizi tu.
“Takwimu zinasaidia mamlaka kubaini bidhaa hatari na kuchukua hatua mapema,” anasema.
Katika ngazi ya sera, maofisa wanasema maboresho yanaendelea. Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Tiba katika Wizara ya Afya, Dk Winifrida Kidima, anasema bidhaa zilizosajiliwa hupitia upimaji wa kisayansi na ufuatiliaji baada ya kuingia sokoni.
“Kupitia Baraza la Tiba za Asili na Mbadala, dawa hupimwa kabla ya kusajiliwa. Ufuatiliaji wa baada ya mauzo hufanyika, na bidhaa zisizokidhi vigezo huondolewa sokoni,” anasema.
Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa udhibiti pekee hautoshi bila elimu kwa umma.
Dk Mushi anasema watumiaji wanapaswa kuhamasishwa kuuliza maswali kuhusu usalama wa bidhaa wanazotumia.
“Hata mmea salama unaweza kuwa hatari ukisindikwa vibaya au ukichanganywa na dawa nyingine. Elimu kwa umma lazima iende sambamba na udhibiti,” anasema.
Ingawa tiba za asili zinaendelea kuwahudumia mamilioni ya Watanzania, wataalamu wanakiri kuwa wapo wanaopata madhara kutokana na matumizi yasiyo salama au yasiyothibitishwa.
Wanasema kuimarisha mnyororo wa usambazaji kunahitaji hatua katika kila ngazi, kuanzia uvunaji, usindikaji na usambazaji hadi matumizi.
“Kama mnyororo ulivyo, uimara wake hutegemea kiungo dhaifu zaidi. Dosari yoyote, iwe katika uvunaji, usindikaji au usambazaji, inaweza kusababisha madhara ya kiafya,” anasema Dk Nyankunga.
Watafiti wa MUHAS wanasisitiza kuwa sayansi inapaswa kuwa kitovu cha mustakabali wa sekta hii. Dk Mugaka anasema tiba za asili zinaweza kuishi sambamba na tiba za kisasa kwa usalama iwapo viwango vitazingatiwa kwa uthabiti.
“Tiba za asili zinaweza kuwa salama na zenye ufanisi, lakini tu pale kila hatua inapozingatia sayansi na udhibiti. Maslahi ya kibiashara kamwe yasizidi usalama wa mgonjwa,” amesema.
Sehemu ya mwisho.