
Balozi wa Palestina nchini Uingereza Husam Zomlot amesema, nchi ya Palestina ipo, imekuwepo siku zote na itaendelea kuwepo daima.
Zomlot ameyasema hayo mbele ya umati wa watu waliokuwa wamekusanyika mbele ya jengo la ofisi ya uwakilishi wa Palestina nchini Uingereza katikati mwa jiji la London katika hatua ya kuashiria ofisi hiyo kubadilika kuwa Ubalozi rasmi wa Palestina nchini humo.
“Tumekusanyika leo mbele ya ofisi ya uwakilishi wa Palestina nchini Uingereza hapa London kuadhimisha lahadha ya kihistoria,” amesema balozi huyo wa Palestina na kubainisha: “katika mji mkuu uleule wa Azimio la Balfour na baada ya kupita zaidi ya karne moja ya kuendelea ukanushaji, upokonyaji na ufutaji, hatimaye serikali ya Uingereza imechukua hatua iliyopitiwa na muda mrefu ya kuitambua nchi ya Palestina”.
Akiwa ameinua bango, Zomlot amesema huku akishangiriwa na umati huo: “hivi karibuni, huku tukingojea baadhi ya taratibu za kisheria, baadhi ya hatua za urasimu … bango hili, linalosomeka ‘Ubalozi wa Nchi ya Palestina’ … litawekwa nyuma yangu kwenye jengo hili.”
Balozi wa Palestina mjini London ameendelea kubainisha kuwa lahadha hiyo “haiihusu Palestina pekee, lakini inaihusu pia Uingereza na dhima nzito iliyonayo serikali ya Uingereza”.
“Ni kuhusiana na kuhitimisha kuwanyima watu wa Palestina haki isiyoweza kupokonyeka ya uhuru na mamlaka ya kujitawala na ni kutambua (Uingereza) dhuluma ya kihistoria (iliyotendeka)”, amesisitiza Zomlot.
Balozi wa Palestina nchini Uingereza amemalizia hotuba yake hiyo kwa kusema: “mabibi na mabwana, nchi ya Palestina ipo, imekuwepo siku zote na itaendelea kuwepo daima”…/