Mahakama ya Sudan Kusini leo Jumatatu imeanza kusikiliza kesi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar, ambaye amefutwa kazi na hasimu wake wa miongo kadhaa, Rais Salva Kiir, huku akikabiliwa na mashtaka kadhaa yakiwemo ya mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya binadamu yanayohusishwa na uasi na shambulio lililofanywa na wanamgambo wanaojulikana kama Jeshi Jeupe.

Machar na washtakiwa wenzake wengine saba ambao wamefunguliwa mashtaka pamoja naye, akiwemo Waziri wa Mafuta, Puot Kang Chol, walionekana wakiwa wameketi ndani ya kizimba kilichofungiwa ndani ya ukumbi wa mahakama wakati wa kesi hiyo ilipokuwa ikionyeshwa mubashara kwenye televisheni ya taifa.

Makamu huyo wa rais wa Sudan Kusini aliyeuzuliwa, alikuwa amewekwa kwenye kizuizi cha nyumbani kwa muda wa miezi kadhaa katika makazi yake mjini Juba.

Mapema mwezi huu, amri ya rais iliyosomwa kwenye redio ya serikali ilisema Kiir amemsimamisha kazi Machar kutokana na mashtaka yanayomkabili ya tuhuma za kuhusika katika mashambulizi yaliyofanywa na Jeshi Jeupe dhidi ya vikosi vya serikali mwezi Machi mwaka huu.

Serikali ya Juba inadai kuwa, Jeshi Jeupe la vijana wenye silaha, lilishambulia kambi ya jeshi huko Nasir, kaskazini mashariki mwa Sudan Kusini, na kuua zaidi ya wanajeshi 250 kwa amri ya Machar.

Chama cha Machar, Harakati ya Ukombizi ya Watu wa Sudan/ Jeshi upande wa Upinzani (Sudan People’s Liberation Movement/Army-in Opposition) (SPLM/IO), kimesema mashtaka hayo ni “ya kubuni” na kwamba wanachama wake walikamatwa kinyume cha sheria. 

Mawakili wa kiongozi huyo wamedai kwamba mahakama hiyo haina sifa zinazostahiki na kwa hivyo haina mamlaka juu ya suala hilo. 

Machar na Rais Salva Kiir wamekuwa hawana mahusiano mazuri. Kiir anatoka kwenye kabila kubwa zaidi la Dinka, na Machar anatoka kwenye kabila la Nuer, ambalo ni la pili kwa ukubwa nchini Sudan Kusini…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *