Mahakama ya Rufani iliyoketi Shinyanga imetupilia mbali rufaa aliyoiwasilisha Rashid Bugali, aliyekuwa akipinga adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya kumuua mkewe, Magreth Kidiga, kwa kumkata sehemu mbalimbali za mwili wake kwa panga.

Mahakama hiyo ya juu nchini imebariki adhabu hiyo dhidi ya Rashid, ambaye akihojiwa na polisi alikiri kumuua mkewe kwa kumkata na panga, akimtuhumu kumuibia fedha kiasi cha Sh 300,000.

Hukumu hiyo iliyobariki adhabu hiyo dhidi ya mrufani huyo imetolewa Februari 19, 2026 na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo ambao ni Shaban Lila, Issa Maige, na Latifa Mansoor, waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo namba 251/2023.

Jaji Mansoor amesema mahakama hiyo, baada ya kupitia mwenendo na sababu za rufaa, imejiridhisha kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka Mahakama Kuu wakati wa usikilizwaji wa kesi ulithibitisha kuwa mauaji hayo yalikuwa ya kukusudia na si ya kujilinda kama alivyodai mrufani.

Awali, mrufani huyo alihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama Kuu Oktoba 5, 2022, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu, ambapo alidaiwa kumuua mkewe Agosti 6, 2018, katika Kijiji cha Ngongwa, Wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu.

Mauaji Yalivyotokea

Wakati wa usikilizwaji wa kesi ya msingi, upande wa Jamhuri ulidai kuwa mrufani alimuua mkewe kwa kutumia panga kwa madai kuwa amemuibia Sh 300,000.

Ili kuthibitisha shtaka hilo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano na vielelezo vitatu.

Shahidi wa kwanza alikuwa Hollo Jibenya, shangazi wa mrufani aliyeshuhudia mauaji hayo ya kikatili. Shahidi wa pili alikuwa Mikael Zakaria, ndugu wa mrufani, aliyeshuhudia mwili wa marehemu ukiwa umefunikwa.

Shahidi wa tatu alikuwa kiongozi wa mtaa huo, John Lwenge, huku shahidi wa nne, Dk. Richard Shija, aliyechunguza mwili huo, alieleza mahakama kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha makubwa kwenye shingo ya nyuma, kichwani, mabegani, na mkononi.

Alidai kuwa majeraha hayo yalikuwa makubwa kiasi cha kusababisha kutokwa na damu nyingi na kifo cha marehemu.

Shahidi wa tano, aliyeandika maelezo ya onyo ya mrufani, aliieleza mahakama kuwa mrufani alikiri kumuua mkewe kwa panga kisha akakimbia na kukamatwa mwezi mmoja baadaye mkoani Shinyanga.

Ilidaiwa kuwa marehemu alichukua fedha hizo kutoka kwa mrufani, jambo lililosababisha mzozo baina yao.

Hata hivyo, ushahidi ulionesha kuwa usiku wa tukio, wakati marehemu akiwa amelala chumbani pamoja na shahidi wa kwanza, mrufani aliingia chumbani humo akiwa na panga.

Shangazi huyo aliieleza mahakama kuwa mrufani alimwamuru atoke nje ya chumba hicho kisha akaanza kumshambulia marehemu kwa mapanga mfululizo, akikatwa kichwani, shingoni, mgongoni na mkononi huku damu ikitiririka kwa wingi.

Aidha, ushahidi wa polisi ulionyesha kuwa mrufani alitoa maelezo ya onyo yaliyopokelewa kama kielelezo mahakamani, ambapo alikiri kumkata mkewe kwa panga na baada ya tukio alitoroka.

Mahakama Kuu iliridhika kuwa upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi thabiti uliothibitisha kuwa mrufani alimuua mkewe kwa nia ya makusudi, na hivyo kumtia hatiani na kumhukumu kifo kwa kunyongwa.

Akijitetea mahakamani, mrufani alidai kuwa alimuua mkewe ili kujilinda baada ya mkewe kumshambulia kwa mchi.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo aliona kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kuwa mrufani alitenda kosa hilo na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Katika rufaa ya sasa, mrufani alikuwa na uwakilishi wa wakili na sababu yake moja ya rufaa ilikuwa kwamba Mahakama Kuu haikuzingatia utetezi wake kwamba mauaji hayo hayakufikiriwa kwani alikuwa akijitetea.

Alidai kuwa mrufani na marehemu walikuwa mume na mke lakini ndoa yao haikuwa ya amani kwani walikuwa wakipigana kila wakati kutokana na mkewe kumwibia fedha.

Alidai siku ya tukio, mkewe alimuibia fedha hizo na kuzihamishia kwenye simu yake ya mkononi, na kuwa mkewe (marehemu kwa sasa) alikuwa mkali na kumshambulia mrufani kwa mchi mzito wa gogo, na kwamba alilazimika kutumia panga kujinusuru.

Kwa hoja hiyo, wakili wake aliomba mahakama ipunguze kosa kutoka mauaji ya kukusudia hadi kuua bila kukusudia, akisisitiza kuwa hakukuwa na nia ya awali ya kuua.

Hata hivyo, Jamhuri kupitia mawakili wake wa serikali walipinga rufaa hiyo, wakieleza kuwa ushahidi wa mashahidi ulionyesha wazi kuwa marehemu alikuwa amelala na hakuwa na silaha wakati mrufani alipovamia chumba hicho usiku akiwa na panga.

Mawakili hao walieleza msimamo wa Jamhuri na kupinga rufaa hiyo hivyo kuunga mkono hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu.

Walidai kuwa Mahakama Kuu ilizingatia utetezi wa mrufani kwa usahihi, kwani hakukuwa na mapigano kati ya mrufani na marehemu wakati mrufani alipomshambulia marehemu kwa panga.

Alidai kwamba shambulio hilo lilitokea usiku wakati marehemu na shahidi wa kwanza walikuwa wamelala, na shahidi huyo aliyeshuhudia zima hakusema kulikuwa na mapigano.

Shahidi wa kwanza alithibitisha kwamba mrufani aliingia chumba ambacho alikuwa amelala pamoja na marehemu, ambapo alimwomba atoke nje na alishuhudia mrufani akimkata marehemu kwa panga sehemu tofauti za mwili wake.

Shahidi huyo alithibitisha kuwa mrufani na mkewe walikuwa na ugomvi kuhusu pesa, lakini mgogoro huo haukuwa sababu ya kujilinda.

Uamuzi wa Majaji

Jaji Mansoor amesema kuwa rufaa ya kwanza ilikuwa na wajibu wa kupitia upya ushahidi wote uliotolewa Mahakama Kuu.

Majaji walibainisha kuwa hakukuwa na ubishi kuhusu kifo cha marehemu wala kuhusu nani aliyesababisha kifo hicho, kwani mrufani mwenyewe alikiri kumkata mkewe kwa panga.

Suala pekee lililohitaji uamuzi lilikuwa kama kitendo hicho kilifanywa kwa kujilinda au kwa nia ya kuua.

Mahakama ilieleza kuwa ili utetezi wa kujilinda ukubalike, ni lazima kuwepo hatari ya karibu inayomlazimisha mtu kutumia nguvu za kujilinda, na nguvu hizo ziwe za kiasi na zinazolingana na tishio.

Katika kesi hiyo, mahakama iliona kuwa mrufani ndiye aliyekuwa mvamizi, aliingia chumbani usiku akiwa na silaha hatari, akamkata marehemu mara kadhaa katika sehemu mbalimbali za mwili.

Majaji walisisitiza kuwa majeraha mengi kichwani na shingoni yanaonesha nia ya kuua, huku wakizingatia mwenendo wa mrufani baada ya tukio, ikiwamo kukimbia eneo la tukio na kukamatwa mwezi mmoja baadaye, jambo walilolitafsiri kama dalili ya hatia.

Mahakama ilihitimisha kuwa hakukuwa na ushahidi wa shambulio lolote lililomhatarisha mrufani wakati wa tukio, hivyo hoja ya kujilinda haikuwa na msingi wa kisheria.

Kutokana na tathmini hiyo, Mahakama ya Rufani ilieleza kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha vipengele vyote vya kosa la mauaji chini ya kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, na kwamba adhabu iliyotolewa na Mahakama Kuu ilikuwa sahihi kisheria.

Rufaa hiyo ilitupiliwa mbali kwa ujumla wake, na hukumu ya kifo kwa kunyongwa kuthibitishwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *