
Polisi nchini Malawi imewatia mbaroni maafisa wanane wa uchaguzi wanaotuhumiwa kujaribu kudukua matokeo ya uchaguzi wakati zoezi la kuhesabu kura likiendelea kufuatia ucaguzi mkuu wa Jumanne iliyopita nchini humo.
Peter Kalaya Msemaji wa Polisi ya Malawi ameeleza katika taarifa kuwa maafisa wanane wa uchaguzi wakiwemo makarani wa masuala ya data na afisa msimamizi wa uchaguzi walikamatwa jana Jumamosi katika eneo bunge la Nkhoma katika maeneo ya mashambani ya mji mkuu, Lilongwe.
“Tayari tumeanzisha uchunguzi ili kubaini hatua hii imetekelezwa kwa lengo na kwa manufaa ya nani. Kwa hiyo tunatoa wito kwa wananchi kuwa watulivu wakati tunasubiri matokeo rasmi ya uchaguzi,” amesema Kalaya.
Jumanne iliyopita wananchi wa Malawi milioni 7 waliotimiza masharti ya kupiga kura walielekea kweye masanduku ya kupiga kura ili kuwachagua Rais mpya, wabunge na magavana watakaotumikia nchi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Hata hivyo, tangu wakati huo hadi sasa, Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) bado haijatangaza matokeo rasmi ya uchaguzi, hatua iliyokosolewa na wadau wakuu wa uchaguzi ambao sasa wanaishinikiza tume kutangaza wazi matokeo ya uchaguzi kwa umma.
Maafisa uchaguzi wa Malawi wamesema kuwa matokeo yamechelewa kutangazwa kutokana na hitilafu za mtandao na kwamba changamoto zilizojitokeza zinaendelea kufanyiwa kazi.
Uchaguzi wa Malawi uliofanyika siku ya Jumanne ulikuwa na ushindani mkubwa kati ya Rais wa sasa wa Malawi Lazarus Chakwera na rais wa zamani Peter Mutharika, ambaye aliondolewa madarakani na Chakwera katika uchaguzi uliopita.