
Upinzani nchini Sudan Kusini umetoa wito wa “mabadiliko ya utawala” dhidi ya serikali ya Rais Salva Kiir baada ya miezi kadhaa ya kuvunjika kwa makubaliano ya kugawana madaraka mwaka 2018 na Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar.
Wito huo umeiweka nchi hiyo katika hatari ya vita vipya vya wenyewe kwa wenyewe. Chama cha Sudan People’s Liberation Movement/Army – Katika Upinzani (SPLM/A-IO) tarehe 15 Septemba pia kilitangaza serikali ya Kiir kuwa “haramu”.
Hayo yanajiri ikiwa ni baada ya wizara ya sheria kupendekeza Machar afunguliwe mashtaka ya uhaini, mauaji na uhalifu dhidi ya binadamu. Machar amekuwa chini ya kifungo cha nyumbani tangu Machi mwaka huu. Baadaye Kiir alimvua Machar wadhifa wake kama makamu wa kwanza wa rais.
Serikali inamtuhumu Machar na washirika wake saba, ambao wanakabiliwa na mashtaka sawa na hayo, kwa “kupanga” mapigano mabaya mwezi Machi kati ya jeshi na wanamgambo wa kabila la Nuer wanaofahamika kama Jeshi la White katika mji wa Nasir kaskazini mashariki mwa jimbo la Upper Nile. Takriban wanajeshi 250 waliuawa katika mapigano hayo.
Hata hivyo, mrengo wa upinzani nchini Sudan Kusini umepuuzilia mbali mashtaka dhidi ya kiongozi wao.
Chama hicho kimesema mashtaka hayo yamebuniwa na yananuiwa kuisukuma nchi katika utawala wa kiimla.
Ikumbukwe kuwa, Machar alikamatwa kwa tuhuma za kujaribu kuchochea uasi mwezi Machi mwaka huu 2015. Mivutano na hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka kati ya pande mbili za Rais Salva Kiir na Machar na ikashtadi mnamo mwezi Februari mwaka huu wakati kundi liitwalo Jeshi Jeupe ambalo ni tiifu kwa Machar, lilipovamia kambi ya jeshi jimboni la Upper Nile na kushambulia pia helikopta ya Umoja wa Mataifa.