Katika taarifa, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani vikali shambulio la jeshi la utawala ghasibu wa Israel dhidi ya raia karibu na hospitali ya Shafa, magharibi mwa Gaza na kulitaja kuwa jinai kubwa ya kivita.
Taarifa ya Hamas inaeleza kuwa, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya wakimbizi waliokuwa wakiondoka katika mji wa Gaza na kupelekea kuuawa shahidi takriban watu 15, yanaonyesha ukatili wa utawala huo unaowaandama raia hata wanapokuwa katika nyakati ngumu za ukimbizi na kuhama makazi yao. Hamas inaichukulia hatua hiyo kuwa muendelezo wa siasa za mauaji ya kimbari za utawala wa Kizayuni dhidi ya taifa la Palestina ambazo zinatekelezwa wazi wazi mbele ya macho ya walimwengu kwa muda wa miaka miwili iliyopita.
Akiashiria ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa kwamba utawala wa Kizayuni umefanya jinai ya mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi wa Palestina, Hamas imesisitiza kuwa jinai hiyo na jinai nyingine za kila siku katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza ni ujumbe wa wazi wa upuuzaji unaofanywa na jamii ya kimataifa na pia ishara hatari ya ukiukaji wa sheria na mikataba ya kimataifa.
Hatua ya utawala wa Kizayuni ya kukanyaga sheria za kimataifa huko Gaza ni suala ambalo taasisi za haki za binadamu, Umoja wa Mataifa na wataalamu wa sheria za kimataifa wamekuwa wakilichunguza na kulitilia mkazo mara kwa mara. Hatua ya jeshi la Kizayuni ya kutumia silaha hatari katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu zikiwemo shule, hospitali na makazi huko Gaza ni kinyume na kanuni ya kutenganisha shahaba za kijeshi na kiraia katika sheria za kibinadamu. Vizuizi vikali vya kuingizwa chakula, dawa na mafuta huko Gaza, ambavyo pia vimesababisha mzozo wa kibinadamu, inachukuliwa kuwa adhabu ya pamoja, jambo ambalo limepigwa marufuku chini ya Mkataba wa Nne wa Geneva.
Utawala wa Kizayuni umekuwa ukipuuza mara kwa mara maazimio ya Baraza la Usalama na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yakiwemo maazimio yanayotaka kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi au kukomeshwa mzingiro wa Gaza. Mara nyingi waangalizi wa kimataifa au waandishi wa habari huru wamekuwa wakizuiwa kuingia katika maeneo ya vita, suala ambalo linawazuia kuandika na kuakili kwa usahihi jinai zinazofanywa na jeshi la Kizayuni katika maeneo hayo. Vitendo hivi vimeharibu miundombinu muhimu ya Gaza na hivyo kuhatarisha maisha ya mamilioni ya Wapalestina.

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limeeleza mara kwa mara katika ripoti zake kwamba, utawala wa Kizayuni umekuwa ukitumia silaha za milipuko mikubwa katika maeneo yenye wakazi wengi katika mashambulizi yake huko Ghaza. Ripoti hizo pia zinazungumzia kunyimwa Wapalestina misaada ya kibinadamu na ukiukwaji wa haki ya uhuru wa kutembea, suala linalochukuliwa kuwa adhabu ya pamoja kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Katika ripoti mbalimbali, Amnesty International pia imeashiria mauaji ya raia wakiwemo watoto na uharibifu wa miundombinu muhimu ya maji na umeme. Pia, matumizi ya nguvu za ziada na kulenga shabaha za kiraia kumeashiriwa kama ukiukwaji wa wazi wa sheria za vita.
Licha ya uungaji mkono wa Marekani na serikali za Magharibi kwa jinai hizo za wazi za utawala wa Kizayuni, lakini katika miezi ya hivi karibuni matukio muhimu yameonekana katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza.
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha azimio ambalo linautia hatiani utawala wa Kizayuni kwa kutekeleza jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu huko Gaza. Katika azimio hilo, matumizi ya njaa kama silaha ya vita yamelaaniwa vikali na nchi zote kutakiwa kuacha kuuzia silaha utawala wa Kizayuni.
Wakati wa mashambulizi dhidi ya Gaza, utawala wa Kizayuni umekuwa ukikiuka wazi sheria za kimataifa na kibinadamu; ikiwa ni pamoja na mashambulizi na mzingiro dhidi ya raia.
Mshikamano wa Ulimwengu wa Kiislamu na waungaji mkono wa Palestina unaweza kuwa moja ya mashinikizi athirifu zaidi ya kukabiliana na jinai za mpangilio za utawala wa Kizayuni dhidi ya raia wasi na hatia. Mshikamano huu sio wa kisiasa na kidiplomasia tu, bali wa kisaikolojia, kihabari na hata kijeshi.
Kwa kutoa uungaji mkono wa kifedha, kimaanawi na kisiasa kwa makundi ya muqawama wa Palestina, nchi za Kiislamu zinaweza kubadilisha mizani ya nguvu na kuzuia kuendelea kukaliwa kwa mabavu Gaza na utawala wa Kizayuni. Uungaji mkono huo pia utaimarisha moyo wa wananchi wa Palestina na kuwafanya wawe wakakamavu zaidi katika kukabiliana na mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni.