Leo ni Ijumaa tarehe 26 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1447 Hijria sawa na Septemba 19, 2025 Miladia.
Miaka 1103 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 26 Rabiul Awwal mwaka 344 miladia aliaga dunia huko Baghdad muhaddith na mtaalamu mkubwa wa masuala ya Kiislamu kwa jina la Ibn Sammak. Historia haijaweka wazi tarehe na mahala alipozaliwa msomi huyo, lakini ripoti zinasema kwamba aliishi mjini Baghdadi, Iraq na kupata elimu na maarifa kwa wasomi wa mji huo. Vilevile historia inasema Ibn Sammak alilea wasomi wengine mashuhuri akiwemo Haakim Nishaburi. Miongoni mwa vitabu vya Ibn Sammak ni kile cha “al Aamali” na vitabu vingine kadhaa kuhusu fadhila na matukufu ya Ahlulbait wa Mtume Muhammad (saw).

Siku kama ya leo miaka 117 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani, alimu na msomi mkubwa wa Kiislamu. Abul-Makaarim Zanjani alizaliwa mwaka 1255 Hijiria mjini Zanjani, kaskazini magharibi mwa Iran ambapo baada ya kuhitimu masomo yake ya awali alielekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kukamilisha masomo ya hawza mjini hapo. Akiwa mjini Najaf, Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani alipata kusoma kwa maulama wakubwa kama vile Morteza Ansari. Aidha baada ya kufariki dunia baba yake, Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani alichukua jukumu la umarjaa wa masuala ya kidini na sheria za Kiislamu hususan mjini Zanjani. Katika kipindi cha mapinduzi ya kikatiba, msomi huyo na kama walivyokuwa wasomi wengine, alisimama kupambana na udikteta wa wakati huo hapa nchini Iran. Vitabu vya ‘Makhaarijur-Rahman’ na ‘Miftaahud-Dhafar’ ni miongoni mwa athari za Ayatullah Abul-Makaarim Zanjani.

Katika siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, serikali ya kwanza huru iliundwa na viongozi wa mapinduzi nchini Algeria. Harakati za wananchi wa Algeria dhidi ya mkoloni Mfaransa zilianza mwanzoni wa Novemba 1954 sambamba na kushika kasi harakati za kupigani uhuru za wananchi hao. Nalo Jeshi la Ukombozi wa Algeria likaundwa kwa shabaha ya kuratibu mapambano. Tarehe 19 Septemba mwaka 1958 serikali ya muda ya Algeria ikatangaza uwepo wake. Hatimaye kushindwa jeshi la Ufaransa kusambaratisha harakati ya wananchi wa Algeria, kulipelekea Algeria ijitangazie uhuru mwaka 1962.

Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, Kuwait na Marekani zilisaini makubaliano ya kijeshi. Makubaliano hayo yalisainiwa karibu miezi sita baada ya Iraq kuhitimisha kuikalia kwa mabavu Kuwait. Viongozi wa Kuwait walidai kwamba, lengo la makubaliano hayo, ni kuzuia kutokea tena uvamizi mwingine wa Iraq dhidi ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya kijeshi, Marekani iliruhusiwa kutumia bandari za Kuwait na kutuma wanajeshi na zana zake za kijeshi katika ardhi ya nchi hiyo na nchi mbili hizo kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi. Mwaka 1991, Kuwait ikatiliana saini makubaliano kama hayo na Uingereza na Ufaransa. Miaka iliyofuatia, Bahrain, Qatar, Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu zilisaini makubaliano ya kijeshi na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Hata hivyo kinyume na matarajio ya viongozi wa nchi hizo za Ghuba ya Uajemi, makubaliano hayo badala ya kuwaletea amani, yalipelekea kutokea ushindani wa kumiliki silaha na kushadidi ukosefu wa amani katika Mashariki ya Kati.
