
Gazeti la Financial Times limeripoti kuwa Umoja wa Ulaya (EU) umeamua kutekeleza mpango wa kuzitumia yuro bilioni 170 milki za Russia inazozishikilia kurudisha “mikopo ya fidia” kwa Ukraine.
Hayo yanajiri wakati huu ambapo EU inakabiliwa na mashinikizo yanayoongezeka ya kutafuta fedha za ziada za kuifadhili Ukraine huku Marekani ikipunguza msaada wake kwa nchi hiyo.
Moscow imelaani kuzuiwa kwa mali zake hizo na kuonya kwamba unyakuzi wowote wa pesa zake utakuwa sawa na “wizi” na kusisitiza kuwa jaribio lolote la kuzitumia mali na milki zake “haitaachwa bila ya jibu”.
Mataifa ya Magharibi yalizuia karibu dola bilioni 300 fedha za Russia baada ya kushtadi mzozo wa Ukraine mnamo 2022. Fedha hizo zimelimbikiza mabilioni ya riba; na nchi za Magharibi zimechunguza njia za kutumia mapato hayo kwa ajili ya kuisaidia kifedha Ukraine.
Mnamo mwaka uliopita kundi la madola makubwa kiuchumi la G7 linalohodhiwa na nchi za Magharibi lilijiepusha kuchukua hatua ya moja kwa moja ya kunyakua mali za Russia, lakini liliunga mkono mpango wa kuipa Kiev dola bilioni 50 za mikopo ili zilipwe kwa kutumia faida iliyotokana na fedha hizo.
Mkuu wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amependekeza kuanzishwa utaratibu wa ‘malipo ya mikopo’, ambayo amesema, inahitajika haraka kuifadhili Kiev.
Hii ni katika hali ambayo, Brussels iko chini ya mashinikizo makubwa ya kugharimia sehemu kubwa ya mahitaji ya Ukraine…/