Boti iliyokuwa ikiwasafirisha wahamiaji 74 ilipatwa na maafa katika pwani ya Libya, na kusababisha vifo vya wahamiaji 61. Taarifa hii imetolewa na Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa( UNHCR).

Taarifa ya UNHCR imeeleza kuwa watu 13 pekee wamenusurika baada ya boti iliyokuwa ikiwasafirisha kuwaka moto katika pwani ya Tobruk kaskazini mashariki mwa Libya tarehe 13 mwezi huu huku wengine 61 wakiwa hawajulikani walipo hadi sasa. 

Msemaji wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) jana alieleza kuwa tukio hili la maafa lilitokea wakati boti ya mpira iliyokuwa imewabeba wakimbizi 74 wa Sudan iliposhika moto katika pwani ya Tobruk, Libya ilipokuwa ikielekea Ugiriki.

UUNHCR imesema kuwa suluhisho la kweli litapatikana ikiwa vita vitahitimishwa nchini Sudan ili familia ziweze kurejea nyumbani salama bila kulazimika kufanya safari hatari kama hizi.

Tangu katikati ya mwezi Aprili 2023, jeshi la Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) wamekuwa wakipigana vita ambapo jitihada kubwa za usuluhishi wa kikanda na kimataifa zimeshindwa kuzaa matunda na kuhitimisha vita hivyo licha ya hali mbaya ya kibinadamu nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *