Chanzo cha picha, Antonov 124
-
- Author, Sharad Ranabhat
- Nafasi, Aviationa2z
Ndege hizi zimeundwa sio tu kusafirisha mizigo mizito lakini pia kupaa kwa kasi na kwa matumizi mbalimbali katika mazingira magumu. Mageuzi katika usafiri wa ndege za kijeshi yamesababisha kutengenezwa kwa ndege kubwa na zenye uwezo mkubwa duniani.
Ndege kubwa ya kijeshi ni muhimu kwa kusafirisha askari, vifaa, magari ya kivita, na misaada ya kibinadamu. Uwezo wa kubeba mizigo, urefu wa ndege, na ukubwa wa mabawa yake, ni vigezo vikuu vinavyofafanua ukubwa huo.
Katika makala haya, tunaangazia Ndege 10 Kubwa Zaidi za Kijeshi zinazofanya kazi kwa sasa, kwa kutazama zaidi uwezo wa kupakia na muundo wa ndege. Tukianza na ya kwanza:
Antonov An-124
Chanzo cha picha, Oleg V. Belyakov-AirTeamImages
Antonov An-124, iliyotengenezwa na Ofisi ya Usanifu ya Antonov ya Ukraine wakati wa enzi ya Usovieti, inasalia kuwa ndege kubwa zaidi ya kijeshi ya usafirishaji duniani kwa uwezo wa kubeba mizigo. Ilianzishwa 1986, inatumiwa na Jeshi la Anga la Urusi na Mashirika ya Ndege ya Volga-Dnepr kwa misheni za kibiashara na kijeshi katika kusafirisha vitu vizito.
An-124 inaweza kubeba hadi tani 150 za mizigo na ina uzito wa kilo 400,000. Umbo lake la ndani lina urefu karibu futi 227 (mita 69.1) na upana wa mabawa ya futi 240 (mita 73.3), ina uwezo wa kusafirisha mizinga, helikopta, na hata ndege nyingine.
Ndege hiyo ina magurudumu mengi ili kutua kwenye njia ambazo hazijatayarishwa vyema. Ndege hiyo imetumika wakati wa operesheni kadhaa za kijeshi na pia inasaidia misheni ya kimataifa ya misaada inapohitajika.
Lockheed Martin C-5M Super Galaxy
Chanzo cha picha, Lockheed Martin
C -5M Super Galaxy ndiyo ndege kubwa zaidi ya kimkakati katika Jeshi la Anga la Marekani. Iliundwa na Lockheed Martin na kuanza kufanya kazi 1969 (kama C-5A), ndege hiyo baadaye iliboreshwa na kuwekwa injini mpya na mifumo yake ya kieletroniki.
Inaweza kubeba mzigo wa takriban tani 130 na uzito wake inapokuwa tayari kupaa ni kilo 381,018. Imeundwa kubeba mizigo na kusafiri mabara bila kujaza mafuta. Urefu wake ni futi 248 (mita 75.5), wakati mabawa yake ni karibu futi 223 (mita 67.9).
Ndege hiyo inajulikana kwa uwezo wake wa kupakia na kupakua mbele na nyuma kwa wakati mmoja. Inasalia kuwa sehemu muhimu ya usafirishaji wa kimataifa na uhamishaji wa haraka kwa Marekani.
Boeing C-17 Globemaster III
Chanzo cha picha, Pixabay
Boeing C-17 Globemaster III ni ndege yenye injini nne iliyoundwa kwa ajili ya Jeshi la Anga la Marekani. Ilianza huduma 1995 na inatumika kwa misheni za kijeshi.
Inaweza kubeba hadi tani 77.5 za mizigo na ina uzito wa kilo 265,352. Umbo lake ndani lina urefu wa futi 174 (mita 53) na mabawa ya futi 170 (mita 51.7). Ina uwezo wa kutekeleza misheni za kudondosha misaada na kutua kwenye njia fupi au zisizo nzuri.
Kwa kuongezea, imetumika sana katika operesheni za kijeshi, Iraqi na Afghanistan, na katika juhudi za kusaidia kupambana na maafa. Inaweza kusafirisha magari, askari, na timu za uokoaji na matibabu.
Xian Y-20
Chanzo cha picha, Ministry of National Defense
Xian Y-20 ni ndege mpya zaidi ya China, iliyotengenezwa na Shirika la Viwanda la Xi’an na kuanza kutumika mwaka 2016. Ndiyo ndege kubwa zaidi ya kijeshi iliyoundwa nchini China hadi sasa.
Ina uwezo wa kubeba tani 66 na uzito wake jumla ni karibu kilo 220,000. Ndege hiyo ina urefu wa futi 154 (mita 47) na ina mabawa ya futi 147 (mita 45). Y-20 inakusudiwa kuongeza uwezo wa Jeshi la Anga la China katika kupeleka vikosi na vifaa umbali mrefu.
China imekuwa ikitumia Y-20 kusaidia kusafirisha vifaa vya jeshi na misaada ya kibinadamu kimataifa. Ndege hiyo inatarajiwa kuboreshwa injini zake katika matoleo yajayo.
Antonov An-22
Chanzo cha picha, Vasiliy Koba via Wikimedia
Antonov An- 22 ilikuwa ndege kubwa zaidi duniani ya turboprop iliporuka kwa mara ya kwanza mwaka 1965. Iliyoundwa na Umoja wa Kisovieti, iliundwa kimsingi kwa ajili ya kupeleka askari kwa njia ya anga na usafirishaji wa mizigo mizito.
Ina uwezo wa kupakia tani 60 na uzito wake kamili ni kilo 114,000. Ndege hiyo ina urefu wa futi 190 (mita 57.8) na mabawa ya futi 211 (mita 64.4). An-22 ina injini nne za Kuznetsov NK-12.
Ndege hiyo ilitumiwa sana kwa usafirishaji katika jeshi la Soviet na baadaye vikosi vya Urusi. Ingawa kwa kiasi kikubwa kazi nyingi zinafanywa na An-124 kwa sasa.
Ilyushin Il-76
Chanzo cha picha, Andrey Rakul
Ilyushin Il-76 ilitengenezwa katika miaka ya 1970 na Umoja wa Kisovyeti ili kupeleka mizigo mizito katika maeneo ya mbali. Tangu wakati huo imekwenda katika zaidi ya nchi 30, zikiwemo Urusi, India, na mataifa kadhaa ya Afrika na Asia.
Uwezo wake wa kawaida wa upakiaji ni tani 50, na uzito wake kamili ni kilo 190,000. Ina urefu wa futi 153 (mita 46.6) na mabawa ya futi 165 (mita 50.5). Ina uwezo wa kupaa au kutua katika njia zisizo na lami na imekuwa ikitumika sana katika usafirishaji wa kijeshi na kiraia.
Il -76 ina uwezo mwingine pia, ikijumuisha uwezo wa kujaza mafuta ikiwa angani na vituo ina vituo vya kamandi ndani yake. Inasalia kuwa muhimu kwa shughuli nyingi za kijeshi na za kibinadamu.
Kawasaki C-2
Chanzo cha picha, Hunini
Kawasaki C-2 ni ndege ya ukubwa wa kati, iliyotengenezwa na Japan ‘s Kawasaki Heavy Industries. Ilichukua nafasi ya ndege ya zamani ya C-1. Hii ya sasa inaweza kusafiri umbali mrefu na ni muhimu kwa Jeshi la Anga la Japan.
Inaweza kubeba hadi tani 37.6 za mizigo na ina uzito kamili wa kilo 141,000. C-2 ina urefu wa futi 144 (mita 44) na ina mabawa ya futi 145 (mita 44.4).
C-2 inatumika kusafirisha askari, vifaa vya kijeshi, na vifaa vya kibinadamu. Japani pia imeuza ndege hizo kwa wanunuzi wa kimataifa kama sehemu ya sekta yake inayokua ya uuzaji wa vifaa vya ulinzi.
Atlasi ya Airbus A400M
Chanzo cha picha, Adrian Pingstone
Airbus A400M Atlas ni ndege ya Ulaya yenye injini nne, iliyotengenezwa na Airbus Defense and Space. Ilianza huduma mwaka 2013 na inaendeshwa na nchi kadhaa za NATO.
A400M inaweza kubeba tani 37 za mzigo na ina uzito jumla wa kilo 76,500. Ina urefu wa futi 148 (mita 45.1) na upana wa mabawa wa futi 139 (mita 42.4).
Ndege hiyo ina vifaa vya kieletroniki vyenye uwezo wa hali ya juu, chumba cha marubani cha kidijitali, na uwezo wa kuongeza mafuta angani na uokoaji. Pia inasaidia kurusha misaada kutoka angani na kutua au kuruka katika uwanja mfupi.
Shaanxi Y-9
Chanzo cha picha, Mil.ru
Shaanxi Y-9 ni ndege ya uwezo wa kati ya jeshi la China. Iliyoundwa na Shirika la Ndege la Shaanxi, ilianza huduma katika miaka ya 2010.
Uwezo wake wa juu wa upakiaji ni tani 30, na ina uzito wa kilo 39,000. Y-9 ina urefu wa futi 118 (mita 36) na ina mabawa ya futi 131 (mita 40). Inaendeshwa na injini nne.
Y-9 inaweza kubeba wanajeshi, mizigo, na magari mepesi ya kivita. Ina uwezo wa kupeleleza pia na kutoa tahadhari.
Lockheed Martin C-130J Super Hercules
Chanzo cha picha, Lockheed Martin
C-130J Super Hercules ni ndege ya uchukuzi inayotumika sana, inatumika na zaidi ya nchi 70. Ni toleo lililoboreshwa la C-130 Hercules, ambayo imekuwa likifanya kazi tangu miaka ya 1950.
C-130J ina uwezo wa kupakia tani 21 na uzito wake ni kilo 74,389. Ina urefu wa futi 113 (mita 34.3) na ina mabawa ya karibu futi 133 (mita 40.4). Ina vifaa vya kieletroniki vilivyoboreshwa, injini mpya za Rolls-Royce AE 2100, na chumba cha marubani cha kidijitali.
Ndege hiyo inatumiwa kusafirisha askari na mizigo, utafutaji na uokoaji, na upelekaji misaada ya kibinadamu. Inaweza kutua au kupaa katika viwanja visivyo na lami na kupaa na kutua katika viwanja vifupi.