Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Phil McNulty
- Nafasi, BBC
Vilabu vyote vya vya Ligi Kuu ya England vimetumia zaidi ya pauni bilioni 2 msimu huu wa joto kusajili wachezaji, na dirisha la usajili litafungwa Jumatatu, 1 Septemba.
Ikiwa imesalia wiki moja, BBC inaangalia usajili wa vilabu sita vikubwa kabla ya tarehe ya mwisho.
Arsenal
Chanzo cha picha, Getty Images
Usajili wa Arsenal ulionekana kuhitimika baada ya kumsajili Martin Zubimendi anayecheza safu ya kiungo na mshambuliaji Viktor Gyokeres, lakini hali ilibadilika baada ya jeraha la goti la fowadi Kai Havertz, na kuwafanya The Gunners kumsajili Eberechi Eze kutoka Crystal Palace.
Chelsea
Chanzo cha picha, Getty Images
Historia inatuambia lolote linaweza kutokea Chelsea kabla ya tarehe ya mwisho, lakini inaonekana kama kocha Enzo Maresca ana nia ya kuimarisha nafasi za mbele, huku Alejandro Garnacho wa Manchester United na mchezaji wa RB Leipzig Mholanzi Xavi Simons, huenda wakajasiliwa.
Mengi yatategemea wanaoondoka, mshambuliaji Nicolas Jackson anatarajiwa kuondoka, pamoja na fowadi mwingine Christopher Nkunku, na winga Tyrique George.
The Blues wanatazamiwa kufikia mauzo ya pauni milioni 270 huku Carney Chukwuemeka na Aaron Anselmino wakisafiri kwa ndege hadi Ujerumani kukamilisha uhamisho wao wa kwenda Borussia Dortmund.
Chelsea pia watajaribu kupunguza kikosi – kwa kumuuza Raheem Sterling na Ben Chilwell – kabla ya tarehe ya mwisho.
Maresca pia anatarajiwa kuimarisha safu ya ulinzi baada ya Levi Colwill kuwa nje kwa muda mwingi wa msimu kutokana na jeraha baya la goti, lakini ametoa ishara kwamba ameambiwa aangalie wachezaji waliopo ndani ya Chelsea ili kutatua tatizo hilo.
Bosi wa Chelsea atalazimika kutatua tatizo hilo bila Renato Veiga kwani beki huyo amekamilisha uhamisho wa kwenda Villarreal kwa ada ya pauni milioni 26.
Liverpool
Chanzo cha picha, Getty Images
Kocha mkuu wa Liverpool Arne Slot amepewa fedha nyingi msimu huu wa joto kumnunu Florian Wirtz, Jeremie Frimpong, Milos Kerkez, Hugo Ekitike na beki chipukizi wa Italia Giovanni Leoni.
Usajili bado utaendelea, huku safu ya ulinzi ya kati ikipewa kipaumbele baada ya kuondoka kwa Jarell Quansah na uhitaji wa Virgil van Dijk kuwa na msaidizi.
Marc Guehi wa Crystal Palace naye analengwa kusajiliwa, baada ya ofa ya pauni milioni 110 ya Liverpool ya kumsajili Alexander Isak wa Newcastle United kukataliwa.
Liverpool bado wanaweza kuangalia kuongeza nguvu upande wa kushoto wa safu yao ya ushambuliaji, lakini kwa sasa hasa wanataka beki wa kati na pengine juhudi nyingine za kumsajili Isak.
Manchester City
Manchester City wamefanya usajili mkubwa, ikiwemo kumsajili kipa James Trafford, kabla ya Kombe la Dunia la Klabu. Na vyanzo vimeiambia BBC Sport kwamba usajili huo umekamilika.
Kumekuwa na uvumi kuhusu kumsajili mlinda mlango wa Paris St-Germain, Gianluigi Donnarumma, lakini hilo litategemea wanaoondoka, huku Galatasaray ikivutiwa kumsajili kipa wa City, Ederson.
Spurs wameonyesha nia ya kutaka kumsajili winga Savinho, jambo ambalo City hadi sasa wamelipinga. Iwapo watamuuza, hilo linaweza kufungua milango kwa City kumnunua Rodrygo wa Real Madrid.
Manchester United
Kocha mkuu wa Manchester United Ruben Amorim ameongeza makali ya timu yake kwa kutumia pauni milioni 200 kununua washambuliaji wapya, Matheus Cunha, Bryan Mbeumo na Benjamin Sesko.
United, hata hivyo, ni wazi wana tatizo kwenye nafasi ya golikipa, Andre Onana akionekana kushuka kiwango na Altay Bayindir akionyesha udhaifu wake kwa makosa wakati wa mechi dhidi ya Arsenal.
Kipa Gianluigi Donnarumma pia anahusishwa na United, lakini mlinda mlango wa Royal Antwerp, Sanne Lammens anaonekana kulengwa zaidi, licha ya kuwa Lammens ameachwa nje ya kikosi cha kwanza cha katika katika mchezo wao wa hivi majuzi dhidi ya Mechelen.
Kocha Amorim pia amekuwa akitafuta nafasi ya kiungo wa kati, lakini nia ya kumnunua Carlos Baleba imesitishwa huku Brighton wakisisitiza kuwa hataondoka.
Uwezekano wa kuondoka Alejandro Garnacho kwenda Chelsea, pamoja na Rasmus Hojlund, ambaye anahusishwa na Napoli, kunaweza kufungua mlango wa usajili zaidi kwa United.
Tottenham Hotspur
Kuondoka kwa Son Heung-min na kuumia vibaya kwa James Maddison kumefungua nafasi za safu ya ushambuliaji, lakini matumaini ni kwamba moja ya nafasi hizo itajazwa na Eberechi Eze wa Crystal Palace yamezimwa na usajili wa Arsenal.
Kumekuwa na mapendekezo ya kumtaka Yoane Wissa wa Brentford, ambaye meneja mpya Spurs, Thomas Frank anamfahamu vyema, lakini dalili zote kufikia sasa ni kwamba anataka kuhamia Newcastle United.
Spurs pia wanaangalia kumsajili Savinho wa Manchester City. Mkataba huo umekwama kwa sasa lakini haitakuwa mshangao ikiwa utaangaliwa upya kabla ya muda wa mwisho kupita.
Ikiwa hilo halitafanyika, Spurs bado watatafuta njia mbadala na wamehusishwa na kiungo mshambuliaji Mfaransa mwenye thamani ya pauni milioni 47.5 Maghnes Akliouche, 23.
Wanaweza pia kuangalia kuongeza watu katika nafasi za ulinzi kwani Radu Dragusin ana jeraha la muda mrefu. Nahodha wa Crystal Palace Marc Guehi, angekuwa chaguo bora lakini Liverpool wanamtolea macho.