
Mahakama kuu ya shirikisho huko Virginia imemfungulia mashtaka Mkurugenzi wa zamani wa FBI James Comey kwa mashtaka mawili yanayohusiana na ushahidi wake kwa Congress.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Bw. Comey, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akikosolewa na Rais Donald Trump, anashutumiwa kwa kusema uwongo kwa Bunge la Congress wakati wa ushahidi wake wa Septemba 2020 kuhusu kama aliidhinisha uvujaji wa habari za siri kwa vyombo vya habari.
Akijibu shtaka hilo, Bw Comey alitangaza kuwa hana hatia na kusema “ana imani kubwa na mfumo wa mahakama ya shirikisho”.
Shitaka hilo linakuja siku chache baada ya Trump kumtaka afisa mkuu wa sheria nchini humo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Pam Bondi, kuwachunguza kwa ukali zaidi mahasimu wake wa kisiasa akiwemo Comey.
Uchunguzi huo unaongozwa na Lindsey Halligan, Mwanasheria wa Marekani wa Wilaya ya Mashariki ya Virginia, ambaye awali alikuwa wakili binafsi wa Trump.
Kesi ya Bw Comey – ambapo mashtaka yanasomwa rasmi mbele ya mshtakiwa mahakamani – imepangwa asubuhi ya tarehe 9 Oktoba huko Alexandria, Virginia saa 10:00 asubuhi kwa saa za ndani, inaripoti CBS, mshirika wa BBC nchini Marekani..
Mwanasheria Mkuu wa Marekani Pam Bondi amesema katika taarifa kwamba hati ya mashtaka “inaonyesha dhamira ya Idara hii ya Haki ya kuwawajibisha wale wanaotumia vibaya nafasi za madaraka kwa kuwapotosha raia wa Marekani”.
Bw. Comey ameshtakiwa kwa kosa moja la kutoa taarifa za uongo na lingine la kuzuia haki.
Idara ya haki iliomba baraza kuu la mahakama kuzingatia mashtaka matatu dhidi ya Comey, lakini ilikubali tu kwamba mawili kati ya hayo yaliungwa mkono na ushahidi wa kutosha kuhukumiwa mahakamani.
Shitaka la tatu lilikuwa shtaka lingine la kutoa taarifa za uongo.
Baraza kuu la mahakama ni kundi la raia lililoundwa na mwendesha mashtaka ili kuamua ikiwa kuna ushahidi wa kutosha wa mashtaka kufunguliwa. Kwa maneno ya kisheria, huamua kama kuna sababu inayowezekana ya kuamini kuwa uhalifu umetendwa.
Yeye ndiye mkurugenzi wa kwanza wa zamani wa FBI kushtakiwa kwa uhalifu, na ameshikilia kuwa hajadanganya chini ya kiapo.
Iwapo atapatikana na hatia, anaweza kufungwa jela hadi miaka mitano.