Katika utafiti huu uliohusisha mataifa 16 ya Afrika ikiwemo Kenya, Tanzania na Ethiopia, zaidi ya sampuli 200 za mbu wa Anopheles Funestus zilikusanywa na kulinganishwa na sampuli za miaka ya 2014, 2018 na hata zile za kihistoria za mwaka 1927.

Dkt. Erick Ochomo, mtaalamu wa wadudu kutoka KEMRI na kiongozi wa utafiti huu, aliambia DW kuwa mbu wameanza kuonyesha tofauti kubwa kulingana na maeneo wanakoishi, jambo linalohusishwa moja kwa moja na mabadiliko ya hali ya hewa.

“Ni aina ya mbu ambao ni vigumu kujua walipo, kwa sababu ni wadogo sana lakini huuma sana sana usiku wa manane. Sasa hivi tabia zao zinabadilika, wanaanza kuuma hata asubuhi na tumewahi kuona wakiuma wanafunzi mashuleni.”

Dkt. Ochomo anasema zaidi ya mabadiliko ya tabianchi, utafiti umeonyesha mbu hawa wakiboresha vinasaba vyao na kujenga kinga dhidi ya dawa. Anafafanua kuwa kati ya mwaka 2000 hadi 2015, visa vya malaria vilipungua kwa kiwango kikubwa nchini Kenya, lakini tangu mwaka 2015 vimekuwa vikibaki katika hali ile ile kwa sababu mbu wameanza kuzoea dawa.

Dawa ya Malaria kwa wachanga yaonyesha matumaini

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

“Kuna maeneo kama Turkana kitambo yalikuwa na malaria wakati wa mvua pekee, lakini sasa kuna malaria miezi yote. Hii ni kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi na vilevile mbu kuzoea madawa. Kila kiumbe duniani kinajitahidi kuendelea kunawiri.”

Hali ya hewa isiyotabirika imechangia mabadiliko ya mifumo ya viumbe

Kwa upande wake, Jeronime Akinyi, afisa wa kijamii anayesimamia mpango wa kudhibiti malaria katika Kaunti za Kakamega na Kisii kupitia shirika la TINADA Youth Action Africa, anasema hali ya hewa isiyotabirika pia imechangia mabadiliko ya mifumo ya viumbe, akisisitiza umuhimu wa elimu kwa jamii kuhusu tabia mpya za mbu.

“Unamtambuaje mbu wa Anopheles? Ukipaa ukutani, huinua mkia juu. Siku hizi hata mchana wanajitokeza, tofauti na zamani walipokuwa huja jioni watu wakiwa majumbani.”

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), malaria bado ni chanzo kikuu cha vifo barani Afrika, ambapo zaidi ya vifo 569,000 viliripotiwa mwaka 2023 pekee. Miongoni mwa mbu wote, Anopheles Funestus anaongoza kwa kusambaza malaria kwa sababu huishi muda mrefu na hupendelea kunyonya damu ya binadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *