Rais wa Marekani kwa mara nyingine tena amekariri katika houba aliyoitoa katika Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa madai yake ya uwongo na yasiyo na msingi dhidi ya Iran.
Kwa mujibu wa Pars Today, Rais mtata wa Marekani Donald Trump amekariri madai yake dhidi ya Iran katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) na kusema kuwa Iran haipasi kumiliki silaha za nyuklia, hata hivyo bila kutaja ukaguzi mkubwa wa mara kadhaa uliofanywa katika wa vituo vya nyuklia vya Iran. Trump amedai kuwa Iran inaunga mkono ugaidi na wakati huo huo akasema wazi kwamba nchi yake imeishambulia ardhi ya Iran kwa kushirikiana na utawala wa Kizayuni.
Trump amedai kuwa alimwandikia barua kwa Kiongozi Mkuu wa Iran na kuituma ili kuweka wazi msimamo wa Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Amesema: Jibu la Iran lilikuwa ni kuendeleza shughuli za nyuklia. Rais wa Marekani bila ya kuashiria kwamba Israel ni utawala pekee duniani ambao haujasaini Mkataba wa Unaopiga Marufuku Uenezaji na Usambazaji wa Silaha Hatari za Nyuklia (NPT) amesema: Inapasa kuanza na Iran ili kuzuia uimarishaji wa silaha za nyuklia. Trump amedai kuwa hakuna nchi yoyote duniani isipokuwa Marekani ambayo imeweza kuharibu taasisi za nyuklia za Iran.

Akiendelea na madai yake ya majigambo na ya kustaajabisha kuhusu kuleta amani duniani, Trump pia alidai kuwa ndani ya miezi saba amefanikiwa kumaliza vita saba visivyoisha baadhi vikiwa vimedumu kwa miaka 31, vita moja miaka 36 na nyingine kwa miaka 28. Amevitaja vita hivyo kuwa ni kati ya Cambodia na Thailand, Kosovo na Serbia, Kongo na Rwanda, Pakistan na India, Israel na Iran, Misri na Ethiopia, Armenia na Jamhuri ya Azerbaijan. Madai haya ya Trump ambayo aliwahi kuyatoa huko nyuma yamekadhibishwa na nchi kama India. Hasa ikizingatiwa kuwa Rais huyo wa Marekani licha ya kuahidi kuhimitimisha vita vya Ukraine kwa siku moja lakini amegonga mwamba katika uwanja huo.
Wakati huo huo, katika hotuba yake hiyo katika Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la UN kama ilivyotarajiwa Trump aliamua kueneza uwongo dhidi ya Iran na kukariri madai yake ya siku zote kwamba Iran inafanya juhudi za kumiliki silaha za nyuklia na kudai pia kuwa Iran inaunga mkono ugaidi.
Sababu ambazo Trump na baadhi ya maafisa wa utawala wake wanasisitiza ili jamii ya kimataifa iamini uwongo wanaosema kuhusu Iran zinaweza kuorodheshwa kama ifuatavyo:
Mosi: Ajenda ya kazi ya kisiasa na kistratejia: Katika kipindi cha urais wake, Trump amejaribu kufungamanisha na kupanga sera za kigeni za Marekani kwa mujibu wa maslahi ya nchi hiyo ingawa kwa mtazamo wake mwenyewe. Moja ya sera hizo ni kuishinikiza Iran kupitia kampeni ya mashinikizo ya kiwango cha juu khususan kuzuia uuzaji nje wa mafuta wa nchi hii na pia kujaribu kupunguza au kuvunja uhusiano kati ya Iran na nchi nyingine duniani. Kwa msingi huo, kwa mtazamo wake anaamini kuwa kutoa tuhuma na madai ya uongo dhidi ya Iran hususan kuhusiana na shughuli za nyuklia za nchi hii na ugaidi ni wenzo wa kushadidisha mashinikizo dhidi ya Tehran ili kuilazimisha ikubali matakwa ya Marekani.
Pili: Kueneza taswira mbovu kuhusu Iran: Katika muhula wake wa kwanza wa urais Trump alipinga vikali makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na kwa kuiondoakwa upande mmoja Marekani katika makubaliano hayo, alijaribu kuidhihirisha taswira hasi dhidi ya Iran mbele ya fikra wa waliowengi duniani. Trump amekuwa akiifuatilia pakubwa mbinu yake hii katika muhula wake wa pili wa urais kwa kupanua kampeni ya mashinikizo ya kiwango cha juu, kueneza chuki na pia kuibua tuhuma mbalimbali dhidi ya Iran. Taswira hii hasi inamuwezesha Trump kustafidi na nyenzo mbalimbali za mashinikizo katika ushirikiano wowote wa baadaye na Iran au katika kuzitaka nchi nyingine kupunguza au kuvunja uhusiano wao na Iran.

Tatu: Kuimarisha uungaji mkono kwa Israel: Sababu nyingine ya kuituhumu Iran katika jukwaa la Umoja wa Mataifa ambapo viongozi wa ngazi ya juu wa nchi wanachama kwa kawaida hushiriki katika hotuba za kila mwaka za marais wa Marekani, ni jitihada za kuhalalisha uungaji mkono wa pande zote kwa utawala wa Kizayuni na pia misaada ya misaada ya kijeshi na silaha kwa utawala huo kwa kisingizio cha kukabiliwa na vitisho vya Iran. Katika kipindi cha uongozi wake, Trump amekuwa muungaji mkono mkubwa wa Israel, na sera zake nyingi zikiwemo za kujiondoa kwa upande mmoja katika makubaliano ya JCPOA na kuiwekea Iran vikwazo zimekuwa zikiwiana na maslahi na malengo ya Israel. Hasa ikizingatiwa kuwa utawala wa Kizayuni siku zote umekuwa ukifanya kila lialowezekana kuidhoofisha na kuitenga Iran na pia kuibua mitazamo hasi kuhusu Iran kimataifa.
Nne: Mitazamo ya ndani: Pia ndani ya Marekani kwenyewe; baadhi ya wasomi wa kisiasa na mirengo maalumu (hasa mirengo mikali ya Republican na miungano ambayo Trump anaungwa mkono na lobi mbalimbali za Kizayuni kama vile AIPAC) wanaipinga vikali Iran na shughuli zake. Kuhusiana na hili, sisitizo la Trump la kujenga taswira hasi kuhusu Iran katika taasisi za kimataifa linaweza kutumika kama wenzo wa kuimarisha uungaji mkono wa ndani hasa kutoka kwa wafuasi wa Republican na lobi za Wazayuni ili kuvutia kura maalumu.
Na mwisho, kwa kuzingatia hatua za kisiasa za Trump na viongozi wengine wa ngazi ya juu wa serikali yake kama Marco Rubio Waziri wa Mambo ya Nje ya Pete Hegseth Waziri wa Vita wa Marekani mkabala wa Iran inaonekana kuwa kuendelea kutoa tuhuma na kuichafua Iran zaidi kunatekelezwa lengo likiwa ni kusogeza mbele malengo ya kijiopolitiki na ya kimkakati ya Marekani hasa kuhusu Iran na pande nyingine wachezaji wa kikanda na pia kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni.