
Katika taarifa yake kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Jenerali Nilforoshan na Sayyed Hassan Nasrallah, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi SEPAH limesisitiza kuwa litaendelea kuwa pamoja na imara na kambi ya Muqawama hadi Palestina na Quds Tukufu zitakapokombolewa.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, sehemu moja taarifa ya kiistratijia ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi viongozi wa Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon na Meja Jenerali Abbas Nilforoshan imesema kuwa, usalama na heshima ya Umma wa Kiislamu ni zao la kujitolea kufa shahidi katika njia ya Muqawama na kupigania haki.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, usalama na heshima iliyopo leo kwa Umma wa Kiislamu na nchi za eneo hili si matokeo ya mazungumzo ya kisiasa na kujidhalilisha mbele ya vitisho vya Wazayuni bali ni kwa sababu ya mujahidina waaminifu na wanamapambano wa Muqawama kumwaga damu zao na kutotereka katika medani ya mapambano.
“Kwa hakika damu ya mashahidi hao inatoa dhamana ya kuendelea kuwepo usalama na kudumisha utulivu na utambulisho wa Kiislamu,” imesema taarifa hiyo.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya kiistratijia ya SEPAH imesema: Uzoefu wa kihistoria na uhalisia wa mambo hadharani unaonesha kwamba Muqawama amilifu na wa kutumia hekima na akili ndilo chaguo pekee linalofaa na la busara kwa ajili ya serikali na mataifa ya eneo hili katika kupambana na siasa za kiistikbari za Uzayuni wa kimataifa.
Pia imesema: Bila ya shaka kulegeza kamba na kukubali kuzungushwa kwenye mazungumzo ya mapatano kutaendelea kuleta fedheha na aibu tu kwa mataifa husika yanayosalimu amri mbele ya vitisho.