
Mwanamume aliyepatikana na hatia ya ujasusi na kutajwa na Iran kama “mmoja wa majasusi muhimu” wa Israel, adui mkuu wa Tehran, ameuawa alfajiri ya Jumatatu, kwa mujibu wa mahakama ya Iran.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Hii ni mara ya kwanza kwa mamlaka ya Iran kutaja jina la mtu huyo, Bahman Choubi Asl. Mahakama haikutoa mara moja tarehe ya kukamatwa kwake.
Vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel vilizuka mwezi Juni, vilivyochochewa na mashambulizi ya Israel dhidi yaIran, ambayo hayajawahi kushuhudiwa, yakilenga maeneo ya kijeshi, mashirika ya serikali na mengine yanayohusishwa na mpango wa nyuklia wa Tehran. Iran ililipiza kisasi kwa mashambulizi ya makombora na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel, taifa lisilotambuliwa na uongozi wa Iran.
Tangu kumalizika kwa mapigano, Iran imeahidi kesi za haraka kwa wale wanaoshukiwa kushirikiana na Israel. Mamlaka ya Iran imetangaza kukamatwa kwa watu kadhaa kwa ujasusi na kunyongwa kwa watu kadhaa waliopatikana na hatia ya kufanya kazi na Mossad, idara ya ujasusi ya Israel.
Mahakama imebainisha siku ya Jumatatu kwamba Choubi Asl alishirikiana “kwa ukaribu” na idara ya ujasusi ya Israel, ikibainisha kuwa “alikuwa na fursa ya kupata hifadhidata muhimu na huru za Jamhuri ya Kiislamu.”
Mashambulizi ya Israel mnamo mwezi Juni yaliua maafisa wakuu wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia, na mamia ya watu wengine, wakiwemo raia. Mnamo Agosti 9, mahakama ilitangaza kufunguliwa kwa uchunguzi wa watu 20 waliokamatwa kwa madai ya uhusiano wao na Israel. Siku chache kabla ya hapo, Iran ilimnyonga Roozbeh Vadi, mwanamume aliyetuhumiwa kupitisha habari kuhusu mwanasayansi wa nyuklia aliyeuawa katika vita hivyo.