
Rais wa Madagascar Andry Rajoelina ameivunja serikali yake siku ya Jumatatu kutokana na kupamba moto maandamano ya upinzani yanayoongozwa na vijana ya kulalamikia uhaba mkubwa wa maji na umeme, mgogoro ambao kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa umesababisha vifo vya watu wasiopungua 22 na kujeruhiwa zaidi ya 100 katika kile kinachotajwa kama changamoto kubwa zaidi kuukabili utawala wake baada ya miaka mingi.
Maandamano hayo, ambayo sasa yameingia kwenye siku yake ya tatu, yalichochewa na hasira zilizotanda ndani ya nchi kutokana na kukatika ovyo umeme na uhaba wa maji ambao unaweza kudumu kwa zaidi ya masaa 12.
Maandamano hayo yameshtadi na kuwa makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa miaka kadhaa katika kisiwa hicho kikubwa zaidi cha Bahari ya Hindi yakichochewa na vuguvugu la “Gen Z” katika nchi za Kenya na Nepal.
Katika hotuba aliyotoa kupitia televisheni, Rajoelina amesema, “ninafahamu hasira, huzuni, na changamoto… Nimesikia wito, nimehisi uchungu.”
Rais wa Madagascar amesema, anaomba radhi ikiwa maafisa wamefeli kutekeleza majukumu yao na kuahidi msaada kwa biashara zilizoathiriwa na uporaji.
Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imethibitisha kwamba maafa yaliyotokea yamesababishwa na hatua za vikosi vya usalama pamoja na kuenea ghasia na uporaji unaofanywa na magenge yasiyo na uhusiano na waandamanaji.
Hata hivyo, wizara ya mambo ya nje ya Madagascar imezikataa na kuzitupilia mbali takwimu zilizotolewa na taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa, ikisema zinatokana na “uvumi au habari potofu.”
Machafuko hayo yanaelezewa kama changamoto kubwa zaidi kwa Rajoelina, kiongozi wa zamani wa mapinduzi ambaye alichukua madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2009 na kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa 2023 uliozusha utata.
Uamuzi wake wa kuvunja serikali unaonekana kama jaribio la moja kwa moja la kuzima ghadhabu na kudhibiti tena hali ya mambo…/