
Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, ameadhimisha miaka 65 ya uhuru wa taifa lake kwa hotuba iliyojumuisha heshima kwa waasisi wa taifa na tathmini ya mageuzi aliyosema yameinusuru nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika kutoka kwenye janga la kiuchumi.
Akizungumza katika mji mkuu wa nchi hiyo, Abuja, siku ya Jumatano, Rais Tinubu alisema kuwa sera zilizotekelezwa tangu alipoingia madarakani mwezi Mei 2023, ikiwemo kuondoa ruzuku ya mafuta ya petroli na kushusha thamani ya sarafu ya kitaifa yaani naira, sasa zinaanza kuzaa matunda. Mageuzi hayo yamekuwa chanzo cha maandamano makubwa kutokana na kupanda kwa gharama za maisha nchini Nigeria.
Rais Tinubu amesema: “Utawala wetu uririthi uchumi uliokuwa karibu kuporomoka, uliosababishwa na miaka mingi ya sera za kifedha zilizopotoshwa na kutokuwepo kwa mwelekeo wa pamoja.”
Ameongeza kuwa serikali yake ilichagua njia ya mageuzi badala ya kuendeleza hali ya kawaida, ni kuwepo uthabiti wa muda mrefu.
Aidha amesema: “Chini ya miaka mitatu baadaye… nina furaha kutangaza kuwa tumefikia mwelekeo mpya. Hali mbaya imepita.”
Amesema uchumi ulikua kwa asilimia 4.23 katika robo ya pili ya mwaka 2025, huku mfumuko wa bei ukishuka hadi asilimia 20.12 mwezi Agosti ambacho ni kiwango cha chini zaidi kwa kipindi cha miaka mitatu. Ametaja ongezeko la uzalishaji wa mafuta ghafi ya petroli, mapato ya rekodi kutoka sekta zisizo za mafuta, na ziada ya biashara kama ishara kuwa Nigeria inapanua uchumi wake zaidi ya mauzo ya mafuta ghafi.
Nigeria ilipata uhuru tarehe 1 Oktoba 1960 baada ya miongo kadhaa chini ya utawala wa kikoloni wa Uingereza , kipindi ambacho wanahistoria wengi wanakielezea kama cha unyonyaji wa kiuchumi, uporaji wa rasilimali, na kukandamiza harakati za utaifa. Baada ya uhuru nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ilikuwa chini ya tawala za kijeshi na vita vya wenyewe kwa wenyewe kabla ya kurejea katika utawala wa kiraia mwaka 1999.
Siku ya Jumatano, Rais Tinubu alikiri kuwa uhuru wa Nigeria umepitia majaribu ya migogoro ya kisiasa na matatizo ya kiuchumi. Alisema kuwa ingawa Abuja haijatimiza ndoto zote za waasisi wa taifa, haijapotea kabisa kutoka kwenye dira yao.
Serikali ya Tinubu imejitahidi kupanua ushirikiano wa kimataifa wa Nigeria na kushughulikia changamoto za kiuchumi zilizodumu kwa muda mrefu. Mwezi Januari, Nigeria ilijiunga na jumuiya ya nchi zinazoibuka kiuchumi, BRICS, hatua ambayo maafisa wa serikali wanaamini inaweza kuimarisha biashara na uwekezaji.