Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, ameonya kuwa shambulio lolote dhidi ya taifa lake litakabiliwa kwa mshikamano wa mataifa ya ukanda, akisisitiza kuwa nchi hiyo katu haiwezi kuwa koloni wala kutawaliwa na nguvu za kigeni.

Akizungumza katika Chuo cha Kijeshi cha Jeshi la Bolivarian mjini Caracas siku ya Jumanne, ambako alitunukiwa shahada ya heshima katika ulinzi wa taifa, Maduro alisema: “Hatutawahi kuwa uwanja wa wakoloni, wala watumwa wa dola lolote la kibabe.”

Alisisitiza kuwa historia ya mapambano ya ukombozi wa bara la Amerika Kusini ni msingi wa mshikamano wa kikanda, akiongeza:

“Iwapo Venezuela itashambuliwa, basi wote tutakuwa tumeshambuliwa. Lazima tuungane kama jeshi moja la ukombozi wa Amerika Kusini kupambana na uchokozi wa kiimla.”

Maduro alieleza kuwa muundo wa kisiasa wa Venezuela una matawi matano ya serikali, huku akisisitiza vyanzo viwili vya ziada vya mamlaka, nguvu ya wananchi na nguvu ya kijeshi, ingawa havijawekwa rasmi katika katiba.

Amesema kuwa mafanikio ya Venezuela katika kukabiliana na vitisho vya nje, ikiwemo hujuma za aina mbalimbali  kutoka Marekani, yametokana na mshikamano wa kitaifa na uimara wa taasisi za ndani.

Rais huyo pia alizungumzia mpango wake wa ‘Mabadiliko Saba’, unaolenga kuimarisha uzalishaji wa ndani kupitia sekta 13 za kimkakati.

Kauli hizi zinakuja wakati mvutano kati ya Venezuela na Marekani ukiendelea, huku Washington ikiendeleza vikwazo dhidi ya serikali ya Maduro. Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, Marekani inapanga kuongeza shinikizo kwa kisingizio cha kupambana na mihadarati.

Hadi sasa, jeshi la Marekani limepeleka meli nane za kivita katika maji ya kimataifa karibu na pwani ya Venezuela, likisaidiwa na ndege za kivita aina ya F-35 zilizotumwa Puerto Rico, katika kile kinachoitwa operesheni ya kupambana na dawa za kulevya.

Jumatano iliyopita, maelfu ya raia walijitokeza Caracas kuonyesha uungaji mkono kwa Maduro na utayari wao kutetea taifa, huku jeshi likionyesha uwezo wake kupitia mazoezi ya kijeshi wakati wa ongezeko la wanajeshi wa Marekani katika Karibiani.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *