Colombia imewafukuza wanadiplomasia wa utawala wa kizayuni wa Israel kwa uchokozi uliofanywa na utawala huo ghasibu wa kuuvamia kijeshi msafara wa kimaataifa wa meli unaojulikana kama Sumud uliokuwa ukielekea Ukanda wa Ghaza kwa ajili ya kufikisha misaada ya kibinadamu; sambamba na imehimiza pia rais wa Marekani Donald Trump afungwe jela kwa ushiriki wa Washington katika mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na jeshi la kizayuni katika eneo hilo la ardhi ya Palestina.

Mapema leo, Rais wa Colombia Gustavo Petro ametoa amri ya kufukuzwa maafisa wote wa kidiplomasia wa Israel walioko Bogota, hatua iliyochochewa, miongoni mwa mambo mengine, na kitendo cha jeshi la utawala huo wa kizayuni cha kuwakamata na kuwaweka kizuizini wanaharakati wawili wa Colombia, waliokuwa kwenye msafara wa meli hizo za misaada.

Wacolombia hao wanawake wametambuliwa kama Manuela Bedoya na Luna Barreto, ambao walikuwa na nia ya kupeleka misaada inayohitajika sana katika Ukanda wa Ghaza kupitia msafara mkubwa wa Sumud wa vyombo 50 vya majini vilivyobeba umati mkubwa wa wanaharakati kutoka nchi kadhaa duniani.

Wanawake wawili hao raia wa Colombia wametiwa nguvuni na jeshi la kizayuni wakati meli waliyokuwemo ndani yake ikiwa maili 150 kutoka pwani ya Ghaza.

Kupitia ujumbe alioweka kwenye mtandao wa X, Rais wa Colombia ameonya dhidi ya kuwekwa kizuizini raia hao wawili wa nchi hiyo na kusema hatua hiyo ni sehemu ya “uhalifu mpya wa kimataifa wa Benjamin Netanyahu.”

Aidha amesisitiza kuwa, ikiwa Rais wa Marekani Donald “Trump ataendelea kuwa mshiriki katika mauaji ya kimbari, kama alivyo hadi leo, hastahili chochote kingine isipokuwa kufungwa jela, na jeshi lake halipaswi kumtii.”

Shambulio dhidi ya msafara wa kimataifa wa misaada kwa ajili ya Ghaza lililoanza jana Jumatano lilishuhudia boti za jeshi la wanamaji la utawala wa kizayuni zikivamia na kukamata meli nyingi za msafara huo, kwa wanajeshi wake kupanda ndani ya meli hizo, na kuwaweka chini ya ulinzi mabaharia na waandishi wa habari walioandamana nao…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *