Mwanaharakati wa mazingira raia wa Uingereza Jane Goodall, ambaye alikuwa mbobezi  katika sayansi ya wanyamapori na hasa uhusiano kati ya sokwemtu na binadamu na kujipatia umaarufu mkubwa duniani kutokana na kazi zake, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 91, taasisi yake imethibitisha.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Katika taarifa iliyotolewa na taasisi yake ya The Jane Goodall, alifariki kwa sababu za asili akiwa mjini Carlifonia ambako alikuwa kwenye ziara ya kuzungumza na wadau kuhusu harakati zake.

Goodall alizaliwa jijini London mwaka 1934, alianza utafiti wake wa kwanza kuhusu sokwemtu nchini Tanzania mwaka 1960, kabla ya mwaka 1977 kuzindua taasisi iliyokuwa ikifanya kazi ya kutoa ulinzi kwa viumbe walioko hatarini kutoweka pamoja na kusaidia miradi ya vijana iliyolenga kuwasaidia wanyama na mazingira.

Goodall ametajwa na viongozi wa dunia kama mtaalamu kiongozi wa masuala ya sokwe mtu, kazi aliyoifanya kwa Zaidi ya miaka 60, huku tafiti zake zikiwa msingi wa kutambua mfanano kati ya nyani na tabia za binadamu.

Tayari viongozi wa dunia akiwemo katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, wamemuelezea Goodall kama mtu mwema na mtafiti ambaye alijitolea kwa sehemu kubwa kulinda viumbe hai na mazingira, kifo chake akisema ni pigo kwa dunia.

Akiwa na umri wa miaka 20 pekee, Goodall alifanya utafiti wa sokwe huko Gombe nchini Tanzania, ambapo alijikita katika kufuatilia tabia za wanyama hao zilizosaidia kutoa changamoto kuwa ni binadamu pekee anayeweza kutumia zana na kwamba sokwe walikuwa hawali nyama.

Wakati wa uhai wake, alitunukiwa tuzo kadhaa ikiwemo ile mjumbe wa Amani iliyotolewa na umoja wa Mataifa mwaka 2002 na baadae kutunukiwa tuzo ya uhuru, tuzo ya juu kutolewa Marekani, akikabidhiwaa na aliyekuwa rais wa taifa hilo, Joe Biden.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *