
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali kitendo cha utawala ghasibu wa Israel cha kuivamia kijeshi msafara wa kimataifa wa meli unaojulikana kama Sumud uliokuwa ukielekea Ukanda wa Ghaza kwa ajili ya kufikisha misaada ya kibinadamu na kuvunja mzingiro Tel Aviv dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Esmail Baqaei leo Alhamisi ametoa taarifa na kueleza kuwa ukatili uliofanywa na Israel unadhihirisha ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na kukitaja kitendo hicho kuwa ni ugaidi.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesifu na kupongeza juhudi za kibinadamu za wanaharakati wa Flotilla na makundi mengine madogo kutoka nchi mbalimbali duniani kusema wanaharakati hao “wamesimama kidete na kudhihirisha mshikamano na watu wa Palestina.
Boti nyingi za msafara wa kimaataifa wa meli zipatazo 50 unaojulikana kama (Sumud) zilivamiwa jana na jeshi la wanamaji la Israel zilipokuwa zikikaribia katika ukanda wa pwani.
Idadi isiyojulikana ya wanaharakati wa msafara huo wa kimataifa walitiwa mbaroni na mawasiliano ya meli hizo na ulimwengu wa nje yalikatizwa na jeshi la lsrael.
Jeshi la Israel limeuvamia kijeshi msafara wa kimataifa wa meli kwa jina la (Sumud) huku utawala huo ukiendeleza mashambulizi na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza. Israel imekuwa ikitumia mzingiro dhidi ya Gaza kama njia ya kushadidisha masaibu na matesa kwa wakazi wa eneo hilo.
Baqaei amesema: Mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya raia wasio na hatia huko Gaza yalidhihirisha wajibu wa kisheria, kimaadili, na wa kibinadamu wa serikali zote duniani kukomesha mauaji hayo na kuwawajibisha wahusika.