Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya (European Political Community – EPC) ni jukwaa jipya la kisiasa lililoundwa mwaka 2022, kwa lengo la kuimarisha mshikamano kati ya mataifa ya bara la Ulaya ndani na nje ya Umoja wa Ulaya (EU).

Wazo la kuanzisha EPC lilitolewa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, katika hotuba yake mjini Strasbourg, kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 2022.

Kwa mujibu wa Macron, Jumuiya hii ilikusudiwa kuleta pamoja mataifa ambayo hayamo ndani ya EU, lakini ambayo yanashiriki maslahi ya pamoja kuhusu usalama, utulivu na maendeleo ya bara hilo.

Mkutano wa kwanza wa EPC ulifanyika Oktoba 2022 mjini Prague, Jamhuri ya Cheki, na ulihudhuriwa na viongozi kutoka nchi zaidi ya 40, akiwemo Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwa njia ya video.

Tangu kuanzishwa kwake, EPC imekuwa jukwaa lisilo la kisheria, bali la kisiasa, ambalo linawawezesha viongozi wa Ulaya kujadili changamoto za dharura bila masharti magumu kama ya Umoja wa Ulaya.

Budapest | Mkutano wa Kilele wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya, EPC
Mikutano ya kilele ya EPC huwaleta pamoja viongozi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya na yale yasio wanachama wa Umoja wa Ulaya.Picha: Filippo Attili/ZUMA Press/IMAGO

Malengo ya EPC

Malengo makuu ya EPC ni kuimarisha usalama wa Ulaya, kukuza ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi, pamoja na kuhimiza mshikamano dhidi ya vitisho vya nje, hasa kutoka Urusi.

Aidha, Jumuiya hii inalenga kushughulikia changamoto za pamoja kama mabadiliko ya tabianchi, usalama wa nishati, uhamiaji na usalama wa kidigitali.

Kupitia mikutano yake, EPC inatoa nafasi kwa nchi zisizo wanachama wa EU kama Uingereza, Norway, Uswisi, Uturuki na mataifa ya Balkan kuhusiana moja kwa moja na viongozi wa EU.

Kwa mfano, Uingereza, ambayo ilijiondoa rasmi kutoka Umoja wa Ulaya kupitia Brexit, sasa inapata nafasi ya kushiriki kwenye mijadala ya Ulaya kupitia EPC bila masharti ya uanachama wa EU.

Kwa Ukraine, EPC ni jukwaa muhimu la kutafuta mshikamano wa kisiasa na kijeshi kutoka kwa Ulaya, katika vita vyake dhidi ya Urusi.

Changamoto na mjadala

Licha ya nia njema, EPC imekumbwa na changamoto, ikiwemo maswali kuhusu uhalisia wa utekelezaji wa maamuzi yake kwa kuwa haina nguvu za kisheria.

Wakosoaji wanasema Jumuiya hii inaweza kuwa tu jukwaa la kisiasa la kutoa matamko bila kuchukua hatua madhubuti, hasa ikilinganishwa na taasisi za EU zenye nguvu za kisheria na kifedha.

Denmark Copenhagen 2025 | Mette Frederiksen na Volodymyr Zelensky wakiwa kwenye mkutano wa Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya
Mkutano ya EPC ilianzishwa kutokana na kitisho hasa kutoka kwa Urusi, kufuatia uvamizi wa taifa hilo dhidi ya Ukraine.Picha: Mads Claus Rasmussen/Ritzau Scanpi/picture alliance

Pia, kuna hofu kwamba EPC inaweza kutumika kama njia mbadala ya kuchelewesha uanachama wa mataifa yanayotamani kujiunga na EU, hususan Ukraine na nchi za Balkan.

Hata hivyo, watetezi wa EPC wanasema kuwa hata kama haina nguvu ya kisheria, umuhimu wake uko kwenye kuimarisha mshikamano wa kisiasa na kuonyesha mshikikano wa Ulaya dhidi ya vitisho vya nje.

Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya imejitokeza kama jukwaa la kipekee linalojumuisha karibu mataifa 50, likionyesha dhamira ya Ulaya kutafuta umoja na usalama wa pamoja katika zama za changamoto kubwa za kisiasa na kiusalama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *