
Zimebaki takribani siku 27 kabla ya watanzania kwenda kufanya maamuzi ya kumchagu rais, diwani na mbunge katika sanduku la kura. Tukiuangalia huo muda tunaweza kusema hizi ni dakika za lala salama, kwani wagombea wamebakiza muda wa chini ya mwezi mmoja tu kabla ya siku ya uchaguzi.
Wakati Oktoba 29 ikisubiriwa kwa hamu, wagombea hao wameendelea kunadi sera zao na kuhakikisha wanatumia mbinu mpya za kuhakikisha vyama vyao vinashika dola na kuliongoza taifa hili la Afrika Mashariki.
DW imezungumza na mgombea mwenza wa Chama cha Upinzani cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) , ambaye amesema kwa muda uliobaki chama hicho kimejinasibu kikisema kuwa kimejikita katika kuzungumza na watanzania na kuwaeleza chanzo cha umaskini wao ni kipi?
CHAUMMA: Tuna uwezo wa kukiondoa chama tawala madarakani
Minja amesisitiza kuwa chama hicho kina uwezo wa kukiondoa CCM madarakanikwa kwa miaka 64 chama hicho hakijaweza kumsaidia Mtanzania. Kuhusu hali ya kiuchumi ya vyama vya siasa wakati wa kampeni, Minja amesema, chama hicho kinaendelea kutafuta fedha za rukuzu kutoka kwa marafiki na wahisani wa chama.
Wakati Chauma wakinadi sera hizo, mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan akiwa mkoani Korogwe na Kilimanjaro amesisitiza kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi. Ama wakati wagombea wakiendelea kunadi sera zao, wananchi nao wametoa maoni yao kuhusu wajibu wao kikatiba wa kupiga kura ifikapo Oktoba 29.
Kwa upande wa Visiwani Zanzibar, mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo,Othman Masoud Othman amewaahidi wakulima wa viungo visiwani humo kuwawekea bei elekezi ili kuwalinda dhidi ya unyonyaji wa madalali na walanguzi.
Na Mgombea urais wa CCM, Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi yeye ameendelea na mbinu za kuwatembelea wananchi katika maeneo yao na kuomba kura akinadi Zaidi sera za uchumi wa bluu, masoko na upatikanaji wa nishati.